Monday, 21 May 2018

 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akifunua kitambaa kuashiria uzinduzi wa mradi wa uunganishwaji umeme wa Gridi ya Taifa kwa mikoa ya Lindi na Mtwara kwenye kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Mahumbika Mkoani Lindi leo Mei 21, 2018. Kushoto ni Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi. Mradi huo sasa umeondoa kero ya muda mrefu ya upatikanaji wa umeme ulio bora na wa uhakika kwenye mikoa hiyo ya Kusini.


NA K-VIS BLOG/Khalfan Said, MAHUMBIKA-LINDI
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amewahakikishia Watanzania wote kuwa Serikali itafikisha umeme kila kona na kila kijiji.

Mhe. Majaliwa aliyasema hayo mara baada ya kuzindua mradi wa uunganishaji wa umeme wa Gridi ya Taifa kwa mikoa ya Lindi na Mtwara kwenye hafla iliyofanyika Kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Mahumbika mkoani Lindi leo Mei 21, 2018.
“Kitendo kinachofanyika hapa leo ni ushahidi wa ahadi ya serikali ya kuwafikishia umeme wananchi wa maeneo yote hadi vijijini na ninachowaomba Watanzania ni kuwa na subira kwani serikali inatekeleza mpango huu wa kuwafikishia umeme awamu kwa awamu.” 
Akizungumzia  uzinduzi huo ambao sasa umetoa suluhisho la uhaba wa umeme kwenye mikoa hiyo ya Kusini, Waziri Mkuu alitoa maagizo kwenye Halmashauri zote mkoani Lindi kuhakikisha maeneo yote nyeti yanayotoa huduma za kijamii kama shule na hospitali yanaunganishiwa umeme.  

“Hatutarajii kuwa na eneo lenye shida ya umeme, hapa ni umeme masaa 24, na umeme wenyewe ni wa kutosha na wa uhakika.” Alisema.

Alisema sera ya serikali ya uchumi wa viwanda,ni kuhakikisha inaweka mazingira wezeshi ili wawekezaji waweze kuwekeza kwenye viwanda.

“Niwaombe  wale watu wanaotaka kuwekeza viwanda vya Korosho, Salfa na vifaa mbalimbali kwenye mkoa wa Lindi sasa ni wakati wao kwenda mkoani humo na kuwekeza kwani hivi sasa kuna umeme bora na wa uhakika.

Aidha Waziri Mkuu aliwaasa wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya umeme, na kuwataka wanapoona vitendo vya watu kuhujumu miundombinu basi watoe taarifa ili wahalifu hao wachukuliwe hatua za kisheria.

“Naomba vifaa vyote vinavyoletwa kwenye maeneo yenu, kwenye vijiji vyenu basi tuvilinde ili hatimaye tuweze kunufaika na uimarishwaji wa miundombinu ya umeme.” Aliasa Waziri Mkuu.

Alisema kupitia Mradi wa REA, yaani umeme vijijini Serikali imepunguza gharama za kuunganishiwa umeme kutoka zaidi ya Shilingi 300,000/= hadi shilingi 27,000/= tu.
“Nitoe wito kwa vijana wa mikoa ya Lindi na Mtwara, sasa changamkieni fursa ya umeme huu, wale wanaofanya kazi za kunyoa, viwanda vya kuchomelea, viwanda vya mbao, watengeneza juice, na shughuli nyingine zote za kiuchumi huu ndio wakati wenu wa kujiinua kiuchumi kupitia umeme.” Alisema
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,(katikati) na viongozi wengine wa serikali wakiwemo mawaziri akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mradi wa kuunganishwa umeme wa Gridi ya Taifa kwa mikoa ya Lindi na Mtwara kwenye kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Mahumbika Mkoani Lindi leo Mei 21, 2018. 
 Waziri Mkuu Majaliwa akimpongeza Waziri Dkt. Kalemani.
 Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, (wapili kulia), akiwa na viongozi wengine, wakiimba wimbo wa taifa baada ya kufanya uzinduzi.
 Waziri Mkuu Majaliwa, na viongozi wengine, akipatiwa maelezo ya ,mradi huo na mmoja wa wataalamu wa TANESCO, kwenye kituo cha Mahumbika.
Waziri Mkuu Majaliwa, akitoa hotuba yake
Waziri Mkuu Majaliwa, akitoa hotuba yake

 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, akitoa hotuba yake
 Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka, akitoa maelezo ya mradi huo.
 Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, akitoa hotuba yake
Waziri Dkt. Kalemani, (katikati), akisindikizwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment