Thursday, 8 February 2018Na Eliphace Marwa – Maelezo

MFUMUKO wa Bei wa Taifa kwa mwezi Januari, 2018 umeendelea kubaki palepale asilimia 4.0 kama ilivyokuwa mwezi desemba, 2017.

Hii inamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Januari, 2018 imekuwa sawa na kasi ilivyokuwakwa mwaka ulioishia mwezi desemba, 2017.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii, Ephraim Kwesigabo(pichani juu) kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu  amesema kuendelea kubaki palepale kwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Januari, 2018 kumechangiwa na bei za baadhi ya bidhaa za vyakula kutobadilika.

“ Baadhi ya bei za vyakula zilizochangia mfumuko wa bei kubaki asilimia 4.0 kati ya mwezi Januari 2017 na Januari 2018 ni pamoja na mahindi kwa asilimia 8.0, maharage kwa asilimia 4.3, samaki kwa asilimia 9.0 na ndizi za kupika asilimia 9.0”, alisema Bw. Kwesigabo.

Aidha Kwesigabo aliongeza kuwa baadhi ya bei za bidhaa zisizo za chakula zilizochangia mfumuko wa bei kwa mwezi Januari, 2018 kubaki palepale ni pamoja na sare za shule kwa asilimia 2.3, huduma za afya katika hospitali binafsi asilimia 10.0, mkaa asilimia 9.4, vitabu vya shule asilimia 2.7 pamoja na gharama za malazi kwa asilimia 3.2.

Vilevile Kwesigabo alisema kuwa kwa upande wa mfumuko wa bei usiohusisha vyakula na nishati kwa mwezi Januari, 2018 umeongezeka kidogo hadi kufikia asilimia 1.4 kutoka asilimia 1.3 kama ilivyokuwa mwezi Desemba 2017.

Kwesigabo aliongeza kuwa mfumuko wa bei nchini una mwelekeo unaofanana na baadhi ya nchi nyingine za Afrika Mashariki ambapo nchini Uganda mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Januari, 2018 umepungua hadi asilimia  3.0 toka asilimia 3.3 kwa mwaka ulioishia mwezi Desemba 2017 na kwa upande wa Kenya kwa mwaka ulioishia mwezi Januari, 2018 umeongezeka hadi asilimia  4.83 toka asilimia 4.50 kwa mwaka ulioishia mwezi Desemba 2017.
Reactions:

0 comments:

Post a Comment