Wednesday, 17 January 2018


Shirika lisilo la kiserikali la Agape AIDS Control Programme (AACP) limetoa mafunzo ya Hisa kwa vijana 15 kutoka katika kata za Mwamalili,Didia na Masekelo zilizopo katika wilaya ya Shinyanga. 


Pamoja na kuwapatia vyeti vya ushiriki wa mafunzo,shirika la AGAPE pia limekabidhi baiskeli 15 kwa vijana 15 walioshiriki mafunzo hayo ambazo zitawamsaidia kurahisisha kusafiri wanapotoa elimu ya hisa katika jamii. 


Mafunzo hayo ya uwezeshaji wa vikundi vya hisa ngazi ya jamii yalianza Januari 11,2018 na kufungwa leo Januari 17,2018 katika darasa la AGAPE AIDS Control Programme lililopo katika kata ya Lubaga katika manispaa ya Shinyanga. 


Mgeni rasmi wakati wa kufunga mafunzo hayo leo,yaliyohudhuriwa pia na maafisa maendeleo kutoka kata hizo tatu,alikuwa Afisa Maendeleo ya Vijana halmashauri ya manispaa ya Shinyanga Charles Luchagula aliyemwakilisha mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro. 
Meneja Miradi wa Shirika la AGAPE Mustapha Isabuda alisema mafunzo yametolewa ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa kuzuia ndoa na mimba za utotoni unaofanywa na shirika hilo kwa kushirikiana na shirika la Firelight. 
“Lengo la mafunzo haya ni kuwawezesha vijana ili wawe wawezeshaji wa vikundi vya kijamii vilivyopo katika maeneo yao ambapo watakuwa wanavipatia ujuzi juu ya faida ya kuweka akiba hasa kupitia mfumo wa Hisa ili kujikwamua kiuchumi”,alieleza Isabuda. 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la AGAPE,John Myola alisema kutokana tafiti mbalimbali kubainisha kuwa umaskini wa kipato ngazi ya kaya huchangia kushamiri kwa matukio ya ndoa na mimba za utotoni,shirika hilo limeamua kuwajengea uwezo vijana ili waweze kujiajiri. 
“Tumetoa elimu ya hisa,ujasiriamali,mpango wa kukopeshana ili wakawaelimishe vijana wenzao na makundi mengine katika jamii kuhusu namna ya kupata mikopo ili kujikwamua kimaisha”,alieleza Myola. 
“Serikali yetu inataka watu wafanye kazi,nasi tunaendelea kushirikiana na serikali,tunataka mabadiliko yapatikane katika jamii,tunahitaji vijana hawa wafanye kazi kwa kujituma kwa kufanya shughuli mbalimbali za kuwaingizia kipato”,aliongeza. 
Aidha aliwataka vijana kutumia akili na nguvu zao vizuri kwa ajili ya kufanya shughuli za maendeleo ili kutokomeza umaskini unaochangia kwa kiasi kikubwa ndoa na mimba za utotoni. 
Kwa upande wake mgeni rasmi,Charles Luchagula aliyemwakilisha mkuu wa wilaya ya Shinyanga,aliwataka vijana hao waliopata mafunzo kuwa mabalozi wazuri katika maeneo yao na kuhakikisha wanaunda vikundi watakavyovitumia kuomba mikopo katika halmashauri za wilaya. 
“Naomba vijana mjiajiri wenyewe ili mpate pesa kwa ajili ya hisa,elimu hii mliyopewa mkaitumie vizuri pia mtunze baiskeli mlizopatiwa kwa ajili kurahisisha usafiri katika maeneo mtakayoyafikia”,alisema. 
“Nitumie fursa hii pia kulipongeza shirika la AGAPE kwa jitihada linazozifanya katika kupambana na ndoa na mimba za utotoni,linafanya kazi kweli kweli bila ubabaishaji,kazi zake zinaonekana na zinapimika”aliongeza. 
Nao washiriki wa mafunzo hayo walilishukuru shirika hilo kwa kuwapatia mafunzo ya hisa na kwamba wataenda kutoa elimu hiyo kwa jamii kama walivyofundishwa kwa kipindi cha wiki moja.
ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Mgeni rasmi ,Afisa Maendeleo ya Vijana halmashauri ya manispaa ya Shinyanga Charles Luchagula aliyemwakilisha mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya hisa kwa vijana 15 na kutoka kata za Mwamalili,Didia na Masekelo zilizopo katika wilaya ya Shinyanga.Aliwasisitiza vijana kufanya kazi kwa kujituma ili kuleta mabadiliko katika jamii.-Picha zote Kadama Malunde - Malunde1 blog
Meneja Miradi wa Shirika la AGAPE Mustapha Isabuda akielezea lengo la mafunzo hayo.Kushoto ni washiriki wa mafunzo hayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la AGAPE,John Myola akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo.Kushoto ni Kaimu Afisa Maendeleo ya jamii halmashauri ya manispaa ya Shinyanga,Aisha Mwinshali.Kushoto ni mgeni rasmi ,Afisa Maendeleo ya Vijana halmashauri ya manispaa ya Shinyanga Charles Luchagula aliyemwakilisha mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro. 
Mgeni rasmi ,Afisa Maendeleo ya Vijana halmashauri ya manispaa ya Shinyanga Charles Luchagula akishikana mkono na mmoja wa washiriki wa mafunzo ya hisa kwa vijana 15 wakati wa kukabidhi vyeti vya ushiriki
Mshiriki wa mafunzo hayo akipokea cheti cha ushiriki
Baiskeli 15 zilizotolewa na shirika la AGAPE kwa ajili ya vijana 15 walioshiriki mafunzo ya hisa.Baiskeli hizo watazitumia wakati wa kutoa elimu katika jamii
Mgeni rasmi ,Afisa Maendeleo ya Vijana halmashauri ya manispaa ya Shinyanga Charles Luchagula akishikana mkono na mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo,wakati akimkabidhi baiskeli atakayoitumia kusafiri akitoa elimu ya hisa kwa jamii
Vijana wakipokea baiskeli
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa katika picha ya pamoja
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Reactions:

0 comments:

Post a Comment