Wednesday, 9 August 2017


NA K-VIS BLOG/Khalfan Said
JUKWAA la Wahariri Tanzania, (TEF), chini ya uenyekiti wake, Bw.Theophile Makunga, limetangaza kuondoa adhabu ya kutoandikwa habari za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda,(pichani juu), kuanzia leo Agosti 9, 2017.
Akitangaza uamuzi huo kwenye hoteli ya Holyday Inn katikati ya jiji la Dar es Salaam leo Agosti 9, 2017, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, (TEF), Bw. Theophil Makunga aliyefuatana na Makamu wake, Bw. Deodatus Balile, Katibu Mkuu, Bw. Neville Meena na Mjumbe wa Kamati Tendaji ya TEF, Bw. Bakari Machum, alisema, baada ya vikao mbalimbali vilivyofanyika baina ya Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam na TEF, wameona ipo haja ya swala la adhabu aliyowekewa Mkuu wa Mkoa kufikia kikomo.
TEF ilivitaka vyombo vya habari vya Radio, Televisheni, Magazeti na Blogs, kutoandakia habari za Mkuu huyo wa Mkoa, kufuatia kile kilichoelezwa kuwa Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul Makonda, aliingia kwenye studio za Clauds Media Group, (CMG), usiku wa Machi 18, 2017, akiwa na walinzi wake waliobeba bunduki, kitendo kilichotafsiriwa na wamiliki wa kampuni hiyo kuwa ni uvamizi.
Hata hivyo TEF, katika mkutano huo na waandishi wa habari imesema, kumekuwepo na mazungumzo ya muda kidogo baina ya Jukwaa la Wahariri na Mkuu wa Mkoa Makonda kutafuta suluhu ya swala hilo, lakini wakati swala hilo linakaribia kutafutiwa ufumbuzi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, akihutubia wakati wa sherehe za uzinduzi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda kuja bandari ya Tanga, alimwita Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, na Mkurugenzi wa vipindi wa Clouds Media Group, (CMG), Bw. Ruge Mutahaba na kuwataka washikane mikono kama ishara ya kumaliza tofauti zao.
“Kwa upande wetu sisi kama TEF tumeona hatuna sababu ya kuendelea kumfungia RC Makonda, wakati tayari Rais amekwisha wasukuhisha watu hawa hadaharani.” Alisema Makunga wakati wa mkutano huo na Waandishi wa habari.
Kama bado kuna tofauti ndogondogo baina yao nadhani wataendelea kujadiliana lakini kwa upande wetu tunasema adhabu imefikia ukomo leo. Alisisitiza makunga.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alisema, yeye na Clouds wamekuwa na mahusiano mazuri kwa muda mrefu na kwamba mazingira ya wakati ule alipoingia kwenye studio za Clouds na walinzi yalikuwa hayaepukiki, kwani walinzi aliopewa wapo kuhakikisha usalama wake, lakini pia kufuatilia nini anachofanya katika katika shughuli zake mbalimbali kama Mkuu wa Mkoa. “ Mimi niseme tu kwamba yaliyopita sindwele tugange yajayo na ninawaomba Waandishi wa habari tuendelee kuwatumikia wananchi wa Moa wa Dar es Salaam kwa kujenga ushirikiano.” Alisema Mhe. Makonda.
Katika mkutano huo pia alikuwepo Bw. Ruge ambaye yeye alisema, haoni sababu ya kuendelea kwa mgogoro huo kwa vile kama ambavyo kauli ya Rais wa Nchi aliyosema kwenye mikutano yake kuwa yeye ni dereva na dereva pengine wakati akiendesha gari amesikia abiria wake wanapiga kelele na ndiyo maana ameamua kuingilia kati na kwa hali hiyo kwa upande wake anaona ni hatua nzuri ambayo sasa hakuna sababu tena ya kuendelea kujadiliana na wala hakuna haja ya kuanza kuuliza nani alikosa na nani yuko sahihi.

 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda, (katikati), akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari ulioitishwa na TEF kwenye Hoteli ya Holyday Inn jijini Dar es Salaam, leo Agosti 9, 2017. Wengine kutoka kushoto ni Bw. Bakari Machum, Mjumbe wa TEF, Bw. Theophil Mkunga, Mwenyekiti wa TEF, Bw. Deodatus Balile, Makamu Mwenyekiti wa TEF, na Bw. Ruge Mutahaba, Mkurugenzi wa Vipindi wa Clouds Media Group, (CMG).
 Bw. Theophil Makunga, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, (TEF), akizungumza leo Agosti 9, 2017.
 Bw. Ruge Mutahaba, Mkurugenzi wa Vipindi wa Clouds Media Group, (CMG), akizungumza leo Agosti 9, 2017.
 Waandish wa Habari wakiwa na "zana" zao.
 Waandishi wa Habari
  Waandishi wa Habari
  Waandishi wa Habari
 Katibu Mkuu wa TEF, Bw. Nivelle Meena, akizungumza leo Agosti 9, 2017
 Bw. Hamisi Mzee kutoka Baraza la Habari Tanzania pia alikuwepo.
 Bw. Balile, (katikati), akitoa ufafanuzi mbele ya Mkuu wa Mkoa Mhe. Makonda, (kushoto), na Bw. Ruge Mutahaba
 Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul Makonda, (kulia), akipeana mikono na Mkurugenzi wa Clouds Media Group, Bw. Ruge Mutahaba, huku Mwnyekiti wa TEF, Bw. Theophile Mkunga, akionyesha furaha yake baada ya kumalizika kwa mgogoro huo.
 Mhe. Makonda na Bw. Mutahaba, wakiondoka kwenye chumba cha mkutano
Mkuu wa Mkoa Makonda (katikati), akijadiliana jambo na Mwenyekiti wa TEF, Bw. Makunga (kushoto) na Makamu Mwenyekti wa TEF, Bw. Balile.
Reactions:

0 comments:

Post a Comment