Friday, 11 August 2017

4
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Doto James (wakwanza kushoto) akibadilishana mkataba ya makubaliano (Strategic Assistance Agreement) na Mkurugenzi wa Shirika la Misaada la Marekani nchini USAID Andy Karas katika Ofisi za Hazina jijini Dar es Salaam.

1
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Doto James (wakwanza kushoto)akisaini mkataba wa Makubaliano (Strategic Assistance Agreement )na Mkurugenzi wa Shirika la Misaada la Marekani nchini USAID Andy Karas(katikati) kuhusu utoaji wa fedha hizo dola za kimarekani 224 zaidi ya Shilingi 450 tukio lililofanyika katika Ofisi za Hazina jijini Dar es Salaam. Wakwanza kulia ni Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini Dkt. Inmi Patterson akishuhudia
5
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Doto James (wakwanza kushoto) akipiga makofi pamoja na Mkurugenzi wa Shirika la Misaada la Marekani nchini USAID Andy Karas(katikati), na  Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini Dkt. Inmi Patterson mara baada ya kusaini mkataba wa makubaliano (Strategic Assistance Agreement ) katika ofisi za Hazina jijini Dar es Salaam.
6
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Doto James akimshukuru Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini Dkt. Inmi Patterson mara baada ya kusaini mkataba huo utakaowezesha Tanzania kupatiwa fedha hizo.
7
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Doto James akimshukuru Mkurugenzi wa Shirika la Misaada la Marekani nchini USAID Andy Karas mara baada ya tukio hilo la mkataba wa makubaliano katika Ofisi za Hazina jijini Dar es Salaam.
(PICHA-na Mpiga Picha Wetu)
………………………..
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
Serikali ya Marekani imetiliana saini na Tanzania makubaliano ya kuipatia ruzuku ya Dola za Marekani milioni 225 sawa na zaidi ya shilingi bilioni 550 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kijamii katika sekta za afya, elimu ya msingi, kilimo, maji na usafi wa mazingira.
Tukio hilo limefanyika Ofisi ya Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam ambapo Tanzania imewakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Doto James na kwa upande wa Serikali ya Marekani, makubaliano hayo yametiwa saini na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID), Bw. Andy Karas
Utiwaji saini wa makubaliano hayo umefanyika siku moja baada ya Marekani kupitia Kaimu Balozi wake hapa nchini, Dkt. Inmi Patterson kukutana na Mhe. Rais Dkt John Pombe Magufuli, Ikulu Jijini Dar es Salaam na kumhakikishia kuwa Serikali yake iko tayari kuongeza misaada kwa Tanzania.
Maeneo ambayo fedha hizo zitatumika na kiwango chake kwenye mabano ni mapambano dhidi ya Ukimwi na Virusi vya Ukimwi (Dola milioni 98.2), Malaria (Dola milioni 46), Kifua Kikuu (Dola milioni 5), Uzazi wa Mpango (Dola milioni 26.4), Sekta ya Kilimo (Dola milioni 45), Maji na Usafi wa Mazingira (Dola milioni 9) na Elimu ya msingi (Dola milioni 13.9)

Akizungumza wakati wa tukio hilo lililohudhuriwa pia na Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini Dkt. Inmi Patterson, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, ameishukuru Marekani kwa msaada huo unaolenga kusadia juhudi za Serikali za kuboresha maisha ya wananchi wake.
“Marekani ni rafiki yetu na mdau wetu mkubwa wa maendeleo wa siku nyingi na ninachowaahidi ni kwamba tutatupa jicho kali kuhakikisha kuwa fedha hizi zinatumika kama ilivyokusudiwa na jinsi tulivyokubaliana” Alisisitiza Bw. James

Nae Bw. Andy Karas amesema Serikali na watu wa Marekani kwa ujumla wanafurahishwa na hatua kubwa ya kimaendeleo iliyopigwa na Tanzania na kuahidi kuwa nchi yake itaendeleza uhusiano huo kwa faida ya nchi hizo mbili.
Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini, Dkt. Inmi Patterson, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanikisha upatikanaji wa fedha hizo.
Reactions:

0 comments:

Post a Comment