Thursday, 3 August 2017


Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akikagua eneo la Dampo la Chidaye.
NA K-VIS BLOG, DODOMA
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo ameipongeza Manispaa ya Dodoma kwa usimamizi mzuri wa miradi inayo tekelezwa na Ofisi ya Rais Tamisemi katika Manispaa hiyo ikiwemo kufanikisha ujenzi wa miundombinu ya barabara za Lami pamoja na ujenzi wa Dampo la kisasa.


Naibu Waziri Jafo aliimwagia sifa Halmashauri hiyo kwa usimamizi mzuri uliofanikisha ujenzi huo licha ya kuanza kutumika tangu mwezi Februari mwaka huu.

“Pamoja na kutumika tangu mwezi Februari lakini hakuna chembe ya harufu wala inzi ukilinganisha na madampo mengine hapa nchini,”amesema Jafo

Amependezwa na mfumo mzima uliotumika katika ujenzi wa Dampo hilo ambalo ni miongoni mwa madampo kadhaa yanayo jengwa na Tamisemi katika miji mbalimbali hapa nchini kwa fedha kutoka Benki ya dunia.

Jafo amewataka wataalam wengine kutoka miji mbalimbali kuja kujifunza ili maeneo yote yanapojengwa madampo hayo waige mfano mzuri wa Dodoma.

Jafo ameutaka uongozi wa jiji la Dar es salaam pamoja na manispaa zake kuja Dodoma kujiongezea maarifa wakati wanajiandaa kujenga miradi kama hiyo katika jiji hilo kupitia mradi wa Dar es salaam Metro Politant Development Project (DMDP) ulio chini ya Ofisi ya Rais Tamisemi.

Naibu Waziri Jafo amewataka wanadodoma kutunza miundombinu hiyo ambayo serikali inaingia gharama kubwa kuijenga.

Dampo hilo linatarajiwa kutumika kwa zaidi ya miaka 19 kuanzia sasa.
Kazi ya utupaji taka na ushindiliaji taka ikifanyika ndani ya Dampo la kisasa la Chidaye.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akizungumza mara baada ya kukagua Dampo la Chidaye.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment