Saturday, 22 July 2017

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli na Mbunge wa Kigoma Mjini Mhe.Zitto Kabwe wakiteta jambo baada ya kuweka jiwe la Msingi mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira wa Manispaa ya Kigoma. Mradi huu utakamilika Novemba 30, 2017 na utamaliza tatizo la maji la mji huo kwa kuzalisha lita milioni 41 ikilinganishwa na mahitaji ya mji huo ya lita Milioni 21.
NA K-VIAS BLOG/KIGOMA
KWA wakazi wa Manispaa ya Mji wa Kigoma-Ujiji, watakubaliana na mimi kuwa kero ya upatikanaji maji safi na salama ya kunywa imekuwa ni miongoni mwa kero tatu kubwa na za muda mrefu mkoani humo.
Kero nyingine ambayo sasa imekuwa ni historia ilikuwa ya upatikanaji wa umeme, wakati ile ya miundombinu ya barabara na reli kila mtu anajua ilivyosumbua kwa miaka mingi.
Yumkini kero ya umeme na miundombinu hususan ya barabara sasa inaanza kuondoka, ikabaki kero ya upatikanaji maji.
Jambo lililosikitisha wengi ni kwamba, Manispaa ya Mji wa Kigoma-Ujiji, imebarikiwa kuwa na ziwa lenye maji baridi, ziwa Tanganyika, hivyo swala la uwepo wa maji mkoani humo sio tatizo tatizo kubwa ilikuwa ni miundombinu ya kuhifadhi na kusambaza maji hayo ili kuwafikia wananchi.
Nakumbuka, aliwahi kutokea mbunge mmoja kutoka Chama Tawala CCM, ambaye sasa sijui yuko wapi, naye ni Mhe. Hamilimenshi Kahena Mayonga, mheshimiwa huyu, yeye akifika bungeni, alikuwa hana hoja nyingine bali ni kulilia mambo hayo matatu kila wakati, lakini hadi anamaliza muda wake na kutupwa nje ya siasa za uwakilishi kutoka mkoani humo, hakuna hata kero moja iliyoshughulikiwa hata walipokuja akina Mhe. Kabourou na wengine wengi mambo yalibaki kuwa yale yale hadi ikafikia wakazi wa mji wa Kigoma kutamani kuwa mkoa wao uhame kutoka mipaka ya Tanzania na kuwa kwenye mipaka ya nchi jirani jambo ambalo kwa maoni yangu isingekuwa suluhisho kwani huko kwa wenzetu pengine kuna shida nyingi kuliko zile ambazo wakazi wa mkoa wa Kigoma walizipitia.
Alipokuja Mhe. Zitto Kabwe, ambaye ni Mbunge wa Kigoma Mjini, mwanzo akiwa kama Mbunge wa Kigoma Kaskazini, walau mabadiliko fulani katka kuatatua kero hizi yalianza kuonekana, mwanzo palifungwa mashine mpya ya kufua umeme, na hivyo changamoto ya upatikanaji wa umeme kwenye Manispaa hiyo ikatatuliwa, baadaye, wakati wa utawala wa awamu ya nne chini ya Rais Dkt. Jakaya Kikwete, kero ya pili ya miundombinu ya barabara nayo ikaanza kutatuliwa kwa barabara ya Kasulu, ambayo ndiyo barabara kuu inayotoka mkoani Kigoma kwenda mikoa ya Mashariki na kwingineko nchini nayo ikaanza kuwekwa lami.
Wakati huo Waziri aliyekuwa anashughulikia Ujenzi, alikuwa Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Hata hivyo kuna kipande cha barabara kilisalia kuwa vumbi, na furaha ya wakazi wa Kigoma-Ujiji imerejea tena hapo majuzi baada ya Mhe. Rais kuzindua ujenzi wa kipande hicho cha barabara kilichosalia ili sasa wananchi waweze kusafiri kwenye barabara ya lami mwanzo mwisho kama wenzao wa mikoa mingine.
Lakini jambo mbalo litakuwa kumbukumbu ya kudumu kwa wakazi wa mkoa wa Kigoma kwa Rais wao Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ni hili la sasa la kuzindua mradi wa maji ambao sasa utakuwa umetatua kabisa kero ya upatikanaji wa maji safi na salama tena ya bomba kwa wakazi wa Manispaa hiyo inayosifika kwa kuwa na ardhi nzuri ya kilimo lakini kuwa na wananchi wenye kupenda kufanya kazi. Hongera sana Dkt. Magufuli na hongera Mbunge Zitto Kabwe, wananchi wa Kigoma nina hakika hawatawasahau.
Reactions:

0 comments:

Post a Comment