Tuesday, 11 July 2017


BENNY MWAIPAJA, WFM, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amefanya ziara ya kushitukiza katika eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kuamuru kituo cha Mafuta cha GBP kifungwe hadi hapo kitakapo funga mashine maalumu za kutolea risiti baada ya kubainika hakitumii ipasanyo mashine za kieletroniki za kukusanyia kodi (EFD)

Dkt. Mpango amechukua hatua hiyo baada ya kujionea kituo hicho kikiwa na pampu nne za mafuta lakini kuna mashine moja pekee ya mkononi ya kutolea risiti jambo linasababisha wateja wao wengi kutopewa risiti na hivyo kuikosesha Serikali mapato yake na ni kinyume cha sheria za nchi.

“Sasa nawachukulia hatua ili liwe fundisho kwa wengine wote wanaouza mafuta nchini bila kufuata taratibu, na nitaanza na wewe, biashara yako isimame mpaka mashine zifungwe kwenye kituo chote na utekeleze mara moja” alisistiza Dkt. Mpango

Katika ukaguzi wa Kituo cha Mafuta cha Puma, Dkt. Mpango amesifu utaratibu mzuri uliowekwa na kituo hicho kwa kufunga mashine maalumu za kutolea risiti zilizounganishwa na kila pampu za mafuta kitu ambacho ndicho Serikali inavitaka vituo vyote vya mafuta vitumie mfumo huo

“Kituo hiki kimezingatia sheria sheria kwa kufunga mashine kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali na hapa tunauhakika wa kupata fedha za kuwatumikia wananchi, kinyume kabisa na kituo cha mafuta nilichokifungia, hapa ndio ningeomba Watanzania wanunue mafuta” aliongeza Dkt. Mpango.

Ameiagiza Mamlaka ya mapato Tanzania-TRA kufanya ukaguzi nchi nzima ili kubaini wamiliki wa vituo vya mafuta wanaokiuka maagizo ya Serikali yaliyowataka wafunge mashine hizo maalumu tangu mwaka uliopita.

Waziri wa Fedha na Mipango amewageukia wenye vyombo vya moto wanaonunua mafuta kwenye vituo vya mafuta kote nchini kudai risiti wanapopata huduma ya kuwekewa mafuta kwenye vituo hivyo ili kuokoa fedha za Serikali zinazoishia mikononi mwa wajanja wachache wanaokwepa kodi kwa makusudi na kuikosesha Serikali mapato yake.

Baadhi ya wananchi wamepongeza uamuzi wa Serikali kupitia Waziri wa Fedha na Mipango wa kufanya ziara za kushitukiza kwenye vituo vya mafuta na kutaka hatua hiyo iwe endelevu kwa maafisa wengine wa Serikali ili kukomesha vitendo vya wenye vituo vya mafuta kukwepa kodi ya Serikali

Katika siku yake ya kwanza ya ziara za namna hiyo, Julai 10 mwaka huu, Dkt. Mpango alikifungia kituo cha Mafuta cha Mawenzi kilichoko Kigamboni, Jijini Dar es Salaam baada ya kubaini kuwa kituo hicho kimefunga mashine maalumu za kutolea risiti za kielektroniki lakini hazitumiki na kuamuru kituo hicho kifungwe hadi kitakapo rekebisha kasoro hiyo na kuvionya vituo vya mafuta vya OilCom kufunga mashine za aina hiyo mara moja.

 Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, akizungumza na mmoja wa wasimamizi wa kituo cha mafuta jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kushtukiza kukagua vituo vya mafuta jijini vinavyokiuka taratibu za mauzo kwa kutokutoa risiti za EFDs.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (mwenye miwani) akizungumza na wananchi pamoja na wafanyakazi wa Kituo cha Mafuta cha Puma, kuhusu umuhimu wa kutoa na kudai risiti baada ya kukagua kituo hicho na kuridhika namna mashine za kieletroniki za kutolea risiti zinavyofanyakazi ipasavyo.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), akiwa katika mitaa ya maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam, akizungumza na baadhi ya wakazi wa maeneo hayo kuhusu umuhimu wa kudai risiti wanaponunua mafuta kwenye vituo vya mafuta na kuitaarifu Serikali wanapobaini wamiliki wa vituo hivyo hawatoi risiti za EFD.

 Waziri Mpango akishuhudia jinsi wananchi wanavyohudumiwa kwenye kituo cha mafuta jijini Dar es Salaam leo Julai 11, 2017.


Kulia ni Ally Gidai Mkazi wa Vingunguti akimueleza Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) kero wanayoipata katika vituo vya mafuta ambavyo havitoi risiti kwa kutumia Mashine za kielektroniki za EFDs. Hii ni baada ya Waziri huyo kueleza umuhimu wa kudai risiti katika vituo vya mafuta.
Reactions:

0 comments:

Post a Comment