Wednesday, 12 July 2017

maja
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekabidhi pikipiki 49 kwa vijana wa wilaya ya Ruangwa ili waweze kujiajiri na kujikwamua kiuchumi.
Amekabidhi pikipiki hizo leo (Jumatano, Julai 12, 2017), baada ya kumaliza kuhutubia wananchi kwenye uwanja wa shule ya msingi Likangara.
 Baada ya kukabidhi pikipiki hizo, Waziri Mkuu amewataka vijana hao kuhakikisha wanakuwa waaminifu kwa kufanya kazi kwa bidii ili pikipiki hizo ziwe na tija.
Amesema vijana wanaoendesha pikipiki maarufu bodaboda wanatakiwa kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali.
“Ukiendesha pikipiki lazima uhakikishe kwamba una leseni, bima, vaa kofia ngumu wewe na abiria wako na marufuku kubeba abiria zaidi ya mmoja.”
Wakizungumza baada ya kukabidhiwa pikipiki hizo vijana hao ambao walikuwa wakiendesha pikipiki za watu ambazo hazina tija, wameahidi kufanya kazi kwa bidii.
 Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametembelea mradi wa ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika zahanati ya Nandagala na kuridhishwa maendeleo yake.
Amesema kukamilika kwa majengo hayo kutarahisisha upatikanaji wa haraka wa huduma za afya kwa mama na mtoto. Pia itawapunguzia kutembea umbali mrefu kwenda kufuata huduma hizo katika hospitali ya wilaya ya Ruangwa.
Reactions:

0 comments:

Post a Comment