Saturday, 15 July 2017

Pic 1
Waziri  wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt.  Harrison Mwakyembe (katikati) akiongea na waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam, kushoto ni Katibu Mkuu kutoka Wizara hiyo Prof. Elisante Ole Gabriel na kulia ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Star Times Bw. Xinxing Pang.
Pic 2
Waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Dkt. Harrison Mwakyembe (hayupo katika picha)  alipokuwa akieleza msimamo wa Serikali kuhusiana na Kampuni ya Star Times jana Jijini Dar es Salaam. (Picha na Lorietha Laurence.)
…………………………………………………………………………
Na Lorietha Laurence -WHSUM.
Waziri  wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt.  Harrison Mwakyembe ameunda kamati ya wajumbe 10 kwa ajili ya kufuatilia undani wa  kutopatikana kwa faida kati ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na kampuni ya Star Times kutoka China.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam alisema kuwa kamati hiyo imepewa siku saba kuhakikisha inakuja na taarifa kamili kuhusiana na suala hilo.
 “ nimeipa kamati  hii  muda  wa siku saba ukimalizika siiongezi tena nitatoa labda siku moja mbili kumalizia tu ili inipatie majibu kamili kwa nini kwa miaka yote hiyo hakuna faida”alisema Mwakyembe.
Aidha Dkt. Mwakyemba  anaeleza kuwa uamuzi wa kuunda kamati hiyo ni kutokana na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuonyesha kukerwa na kutokupatikana kwa faida kwenye ushirikiano huo wa TBC na Star Times alipofanya ziara yake mwezi Mei mwaka huu.
 Anazidi kufafanua kuwa Rais alikasirishwa  na kitendo cha kampuni hiyo kufanya kazi nchini kwa kipindi cha miaka saba bila faida  yoyote  na hivyo kuagiza hatua stahiki  kuchukuliwa juu ya suala hilo.
 Dkt. Mwakyembe anabainisha kuwa tangu kutolewa kwa kauli ya Rais Mhe. Dkt. Magufuli Wizara na watendaji wake tayari wameshafanya mikutano miwili mmoja Mjini Dodoma na  mwingine Jijini Dar es Salaam wakajadili kwa kina sababu zinazopelekea kushindwa kupatikana kwa faida.
 Kabla ya mkutano na waandishi wa habari ,Waziri Dkt. Mwakyembe  alitumia takribani saa tatu akijadiliana kwa kina na Mwenyekiti wa Kampuni ya Star Times kutokea nchini China, Xinxing Pang pamoja na wafanyakazi wa wizara akiwamo Katibu Mkuu Profesa Elisante Ole Gabriel na Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo, Dkt.Hassan Abbas.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Star Times Bw. Xinxing Pang alisema kuwa ana imani kuna uwezekano wa kumalizwa kwa suala hilo  kwa kutumia wataalamu wake watakaoangalia sababu za kutokupatikana kwa faida na nini kifanyike  katika kuondokana na changamoto hiyo.
Reactions:

0 comments:

Post a Comment