Friday, 28 July 2017

 Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, akiteta jambo na Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji nchini, Dkt. Anna Makakala wakati alipofanya ziara ya kushtukiza makao makuu ya Uhamiaji Kurasini jijini Dar es Salaam leo Julai 28, 2017 ambapo pamoja na mambo mengine amesema, Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Rais Dkt. John Pombe Magufuli, ameagiza Naibu Kamishna wa Idara hiyo, Bi Grace Hokororo asimamishwe kazi mara moja ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za kuwaingiza nchini raia wa Somalia wapatao 50 kwa kuwapa vibali kinyume cha taratibu. (PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
 Mhe. Majaliwa (katikati), Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba, (kushoto) na Dkt. Makakala.
 Kikao kikiendelea
 Mhe. Majaliwa anapokelewa makao makuu ya Uhamiaji.
 Mhe. Majaliwa akijadiliana jambo na viongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Uhamiaji.
 Mkutano ukiendelea
Picha ya pamoja
Bi. Grace Hokororo


NA OWM, DAR ES SALAAM
RAIS Dkt. John Magufuli amemuagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kumsimamisha kazi Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Bi. Grace Hokororo. Waziri Mkuu alewaambia waandishi wa habari kuwa Bi. Hokororo amesimamishwa  kazi kwa tuhuma za kuingiza nchini raia 50 wa Somalia na kuwapa vibali vya kuishi kinyume cha taratibu.
Kauli hiyo imetolewa leo (Ijumaa, Julai 28, 2017), na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mara baada ya kumaliza kikao na Makamishna wa uhamiaji. Kikao hicho kilifanyika Makao Makuu ya Uhamiaji jijini Dar es Salaam.
Pia Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba kuunda tume ya uchunguzi kuhusu utoaji wa vibali uraia nchini.
Amesema haiwezekani raia wa kigeni wanaingizwa nchini na wanapewa vibali vya kuishi bila ya kufanyiwa uchunguzi wa kina. “Idara ya Uhamiaji tunaitegemea kusimamia mipaka yetu na kuziba mianya ya watu kuingia bila ya kufuata taratibu lakini kwa mapenzi yake Ofisa huyu ameruhusu Wasomali kuingia bila kufuata taratibu.”
Waziri Mkuu amesema ni lazima uchunguzi ufanyike ili kubaini “Tulidhani ni kitu gani kilimsukuma kutoa vibali kwa Wasomali hao ambao hawakuwepo nchini wameingia na kupewa vibali moja kwa moja kwa mapenzi yake tu sasa hii ni dosari hatuwezi  kuivumilia.”
Amesema Serikali inaitegemea Idara ya Uhamiaji kwa kuzuia mianya ya uingiaji raia mbalimbali kutoka nje ya nchi bila ya kufuata taratibu, hivyo Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli ameagiza Ofisa huyo asimamishwe kazi na uchunguzi ufanyike ili kubaini malengo yake.
"Hawa Wasomali aliowapa vibali vya kuishi wala hawakuwa wanaishi nchini wameingia tu na kupewa vibali, hivyo Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli ameagiza ofisa huyo akae pembeni na achunguzwe ni kujua ni kitu gani kilimsukuma kutoa vibali kwa raia hao."
Pia Waziri Mkuu ameiagiza idara ya Uhamiaji wadhibiti kitengo cha utoaji hati za kusafiria za Kibalozi na kwa wanaomaliza muda wasipewe tena. " Lazima hati hizo zikaguliwe katika mipaka yote na maeneo yote ya usafiri ili kujua kama huyo anayeitumia bado anahadhi hiyo na msiporidhika ichukuweni kwani kuna watu wanazitumia vibaya."
Hata hivyo Waziri Mkuu ameagiza uchungilzi wa kina ufanyike kwa watu wote walioomba hati za kusafiria pamoja na vibali vya makazi kama wanakidhi matakwa ya kisheria kabla ya kuwakabidhi.
Reactions:

0 comments:

Post a Comment