Tuesday, 11 July 2017

 Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, (kushoto), akisikiliza kero za wananchi wakati alipofanya ziara ya kushtukiza kwenye ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania, (TRA), huko Vingunguti jijini Dar es Salaam, leo Julai 11, 2017, kujionea jinsi Mamlaka hiyo inavyowahudumia wananchi waliojitokeza kulipia kodi ya majengo. TRA imesogeza mbele zoezi hilo la ulipaji kodi ya majengo hadi Julai 15, 2017 ili kuwawezesha wananchi kufanya hivyo.

NA BENNY MWAIPAJA, WFM, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amefanya ziara ya kushitukiza katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, eneo la Vingunguti Jijini Dar es Salaam leo Julai 11, 2017 na kuagiza kuongezwa kwa wafanyakazi na vitendea kazi katika ofisi hiyo baada ya kukuta msongamano mkubwa wa watu waliojitokeza kulipa kodi ya majengo.

Dkt. Mpango ambaye alitumia muda wake mwingi kusikiliza kero za baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam waliojitokeza kwa wingi kulipa kodi hiyo, ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania kuongeza wafanyakazi kumi pamoja na mashine za kieletroniki za kukusanyia kodi pamoja na kuweka utaratibu mzuri wa kuwahudumia wazee na watu wenye ulemavu.

“Nimeagiza wafanyakazi waongezwe, viti 50 kwa ajili ya kutumiwa na wazee pamoja na akina mama wenye watoto vitaletwa, pamoja na kuongeza mashine za kielektroniki 5 kutoka 3 zilizokuwepo ambapo sasa zitakuwa mashine 8, hatua hii itaondoa changamoto hii” alifafanua Dkt. Mpango

Amerejea pongezi zake kwa Watanzania kwa kujitokeza kwa wingi kila mahali nchini kote kulipa kodi ya majengo akikielezea kitendo hicho kuwa ni cha kizalendo na kitaisaidia nchi kuondokana na umasikini kwa kuwa itakuwa na uwezo wa kuwahudumia wananchi wake kikamilifu.

Dkt. Mpango amewahakikishia Wazee waliotimiza umri wa kuanzia miaka 60 na kuendelea kwamba Serikali imewaondolea kodi ya majengo kwenye nyumba zao wanazoishi kutokana na kutambua mchango wao mkubwa katika kulitumikia Taifa wakati wa ujana wao.

Baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam waliojitokeza kulipa kodi katika Ofisi hiyo ya TRA, Vingunguti, wamepongeza utaratibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Philip Mpango wa kuwajibika na kutumia muda wake kuwatembelea na kuwahudumia wananchi na pia wamemmwagia sifa kem kem Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa hamasa kubwa aliyowapa na kwamba wako tayari kumuunga mkono kwa hali na mali ili nchi ipate maendeleo kwa haraka

Hii ni siku ya pili kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango kufanya ziara za kushitukiza katika maeneo muhimu kwa lengo la kuangalia utaratibu wa ulipaji kodi mbalimbali hususan ya majengo na vituo vya mafuta ili kubaini kasoro mbalimbali na kutoa maelekezo masuala muhimu anayoyabaini ambapo jana alikuwa Kigamboni, Jijini Dar es Salaam.

 Dkt. Mpango (kushoto), akizunguzma na afisa kodi wakati wa ziara hiyo
 Waziri Dkt. Mpango, akizungumza na wananchi walipa kodi kwenye ofisi za TRA Vingunguti jijini Dar es Salaam.
 Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Charles Edward Kichere(kulia), akiangalia jinsi watendaji wake wanavyowahudumia wananchi.
  Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Charles Edward Kichere(kushoto), akizunhumza na mwananchi aliyefika kulipia kodi ya majengo.
 Waziri Dkt. Mpango, akizungumza na wananchi walipa kodi kwenye ofisi za TRA Vingunguti jijini Dar es Salaam.
 Dkt. Mpango akiondoka ofisi za TRA Vingunguti jijini Dar es Salaam, baada ya ziara yake
Dkt. Mpango akiondoka ofisi za TRA Vingunguti jijini Dar es Salaam, baada ya ziara yake
Reactions:

0 comments:

Post a Comment