Tuesday, 11 July 2017


Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (Wa pili kushoto) akitoa maelekezo kwa Mkandarasi anayejenga Kituo cha Mzani cha Singiwe Kilichopo katika barabara ya Sumbawanga-Matai-Kasanga Port (112KM) Mkoani Rukwa  wakati alipokagua ujenzi huo Mkoani Rukwa.


NA  WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO.
SERIKALI kupitia Wakala wa  barabara nchini TANROADS mkoa wa Rukwa imekamilisha ahadi yake kwa wananchi ya kuwapunguzia changamoto ya usafirishaji wa abiria na mzigio kwa kukamilisha ujenzi wa Daraja la mto  Kalambo  pamoja na barabara ya Sumbawanga Matai hadi Kasanga port (112km) ambapo Kilomita 71.4 zimeshawekwa lami.
Akizungumza mara baada ya kukagua daraja na barabara hiyo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutafungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa mkoa Rukwa na nchi nyingine za jirani ikiwemo Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Burundi.
"Tuliwaahidi wananchi kujenga darala  na barabara hii ili wafanyabiashara na wakulima waweze kusafirisha bidhaa na mazao yao kwenda katika masoko kwa wakati na hivyo kukuza uchumi wao binafsi na taifa kwa ujumla,” ameaema Eng. Ngonyani.
Ameongeza kuwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli Serikali itahakikisha ndani ya kipindi cha miaka mitano inakamilisha ahadi zote walizoahidi kwa wananchi ili wananchi wanufaike na Serikali yao.
"Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli ipo kwa ajili ya wananchi wote, na sisi kama wasimamizi tuliopewa dhamana kwenye Wizara tutahakikisha kile tulichokiahidi kwa wananchi  tunakitekeleza kwa wakati ili wananchi wanufaike na uchumi wa nchi ukue,” amesisitiza Eng. Ngonyani.
Kwa upande wake Meneja wa Tanroads Rukwa amewataka wananchi kutunza miundombinu ya barabara na kuacha vitendo vya kung'oa alama za barabarani ambazo zimewekwa ili kuongeza usalama kwa madereva katika matumizi ya barabara hizo.
"Tumeweka alama hizi barabarani kwa ajili ya  kuongoza madereva wanaotumia barabara ili kuepusha ajali zinazoweza kutokea kwa kutokuwepo na alama za tahadhari, hivyo ni wajibu wenu kuzilinda  na kuzitunza  kwani zipo kwa faida yetu sote,” amesema Eng. Msuka Mkina
Katika hatua nyingine Waziri Ngonyani amekagua huduma za bandari ya Katanga ambapo amesema Serikali itaendelea kuziboresha bandari zilizopo ukanda wa ziwa Tanganyika ili kuvutia wasafirishaji wa mizigo mikubwa kutumia bandari hizo.
"Tutaendelea kuimarisha miundombinu ya bandari ya Kalema, Kigoma na Katanga ili ziwe na uwezo wa kupakia na kupakua mizigo mikubwa kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Burundi,” amesisitiza Eng. Ngonyani.
Naye Msimamizi wa Bandari Mkoa wa kigoma, Bw. Morris Mchindiuza amesema Mamlaka ya bandari TPA imejipanga na imetenga kwenye bajeti yake kiasi cha Sh. bilioni 1 kwa ajili ya  upanuzi wa Gati namba moja na hivyo kuchochoa ukuaji wa wa kibiashara na ongezeko la Meli hususani nchi za jirani kama Burundi na DRC Congo.
Naibu Waziri Eng. Ngonyani yupo katika Ziara ya kukagua Miundombinu ya barabara, Viwanja vya Ndege, Ujenzi wa Nyumba za viongozi, huduma za mawasiliano ya simu, Bandari   na Madaraja katika Mkoa wa Rukwa


Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (Wa pili kulia) akipokea taarifa ya ujenzi ya barabara ya Sumbawanga-Matai-Kasnga Port (112KM) Mkoani Rukwa  wakati alipokagua ujenzi huo Mkoani Rukwa.


Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (Wa pili) akielekeza jambo kwa Msimamizi wa bandari ya Kigoma,Bw. Morris Mchindiuza (Wa kwanza) wakati alipokagua huduma za bandari ya Katanga Mkoani Rukwa.Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (aliyenyoosha kidole) akiongea na wakazi wa kijiji cha Katete Wilaya ya Sumbawanga Mkoani Rukwa wakati alipokagua barabara ya Matei-Kasesya (KM).
Reactions:

0 comments:

Post a Comment