Friday, 9 June 2017Magufuli
Na Judith Mhina – MAELEZO
Kufuatia agizo la Rais John Pombe Magufuli la kumtaka Mkandarasi atakayesimamia ujenzi wa Reli ya Standard Gauge kutoa kipaumbe cha ajira kwa vijana wa Kata ya Pugu, wilayani Ilala, tayari maombi ya Vijana 1,218 yamewasilishwa.
Wakielezea wakati wa mahojiano na Idara ya Habari (MAELEZO) ofisini kwao leo kuhusu utekelezaji wa agizo la Rais juu ya ushiriki wa vijana katika shuhguli mbalimbali za ujenzi wa reli hiyo, Wenyeviti wa Serikali za Mitaa katika Kata za Pugu Bombani na Pugu Stesheni wamesema kati ya idadi hiyo, Wanaume ni 945 na Wanawake 273.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Pugu Stesheni Bwana Sifa Makakala amesema katika Kata yake yenye wakazi 7,636 jumla ya vijana wa kike 396 na vijana wa kiume 88 wameomba kufanya kazi katika ujenzi wa Reli ya Stardard Gauge. Aidha, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kinyamwezi Bwana Mkumbo David amesema,  katika Kata yake yenye wakazi 7,573 jumla ya vijana wa kike 25 na wa kiume 35 wameomba ajira.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa “Kwa Mustafa” Bibi Bahati Usinzi amebainisha kuwa, katika Kata yake yenye Wakazi 9,705 wakiwemo wanawake 5,593 na wanaume ni 4,412, jumla ya vijana wa kiume 214 na wa kike 60 wameomba ajira.
Akihitimisha taarifa ya utekelezaji wa agizo la  Rais Magufuli, Mwenyekiti wa Mtaa wa Pugu Bombani, Bwana Gido Lupiana amesema, “Vijana wengi wamepitisha barua zao za maombi ya ajira katika mtaa wangu, lakini kwa bahati mbaya sina kumbukumbu sahihi.” Hata hivyo, kwa makisio amesema jumla ya vijana 100 wameomba  kupitia Mtaa wa Bombani na wengine 300 waliotoka nje ya Mtaa huo na mikoani.
Kwa mujibu Kaimu Mtenda Mkuu wa Kampuni Hodhi wa Mali za reli-RAHCO Bwana Masanja Kadogosi, takriban Wafanyakazi 154 wameajiriwa katika Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Standard Gauge katika vituo vya maandalizi vya Soga na Ngerengere ambapo Mkataba wa ujenzi wa reli hiyo umetamka kuwa ajira za kiufundi asilimia 80 watatoka Uturuki na asilimia 20 Watanzania.
 Aidha, kwa upande wa nguvu kazi na zile za mtambuka, asilimia 80 ya waajiriwa wanatakiwa wawe Wazawa na Asilimia 20 Wageni. Mradi wa reli ya standard gauge una jumla ya nafasi za ajira 6,000 za watanzania.
Kadogosi ametoa wito kwa Wananchi kuwa makini na watu wanaodai kuwa wameingia Mkataba na RAHCO kama wakala wa kuwatafutia watu kazi katika ujenzi wa Reli hyo. “Tumesikia kuna watu wanachukua fedha kutoka kwa wananchi kwa ahadi ya kupatiwa kazi RAHCO.”  Alisisitiza Bw. Kadogosi.
 “Tupo kwenye maandalizi ya kufungua mtandao wa RAHCO, mara utakaofunguliwa tutaweka nafasi zote za kazi pamoja na zile za ukandarasi. Pia RAHCO itaandaa chapisho maalum kwa Wakandarasi wazawa kuwaelezea fursa zinazopatikana ili waweze kuzichangamkia kama alivyosisitiza Rais Magufuli,”Amesema Kadogosi.
Akiwa katika uzinduzi wa ujenzi wa Reli ya Standard Gauge tarehe 12 Aprili mwaka huu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alitoa agizo kuwa, vijana wa Kata ya Pugu Bombani na Pugu Stesheni wapewe upendeleo maalum katika ajira zitakazotolewa na Kampuni ya Ujenzi ya YAPI kutoka Uturuki.
Reactions:

0 comments:

Post a Comment