Friday, 16 June 2017


NA DAUDI MANONGI,MAELEZO
SERIKALI kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais(Muungano na Mazingira), imelenga kupanda miti zaidi ya milioni 280 kila mwaka katika maeneo yaliyo katika hatari za kukabiliwa na hali ya jangwa na ukame.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais(Muungano na Mazingira) Mhe.January Makamba, (pichani katikati), alipokuwa akiongea na Waandishi wa habari leo Juni 16, 2017 mjini Dodoma kuhusu maadhimisho ya Siku ya kupambana  na kuenea kwa hali ya jangwa na Ukame Duniani inayofanyika Juni 17 kila mwaka.

“Ukataji wa miti kiholela na uharibifu wa misitu unaosababishwa na utegemezi  mkubwa wa binadamu wa kupata mahitaji kutokana  na mazao ya misitu pamoja na huduma zingine muhimu,kunazidisha ukubwa wa tatizo hili”,Aliongeza Mhe.Makamba.

Aidha Waziri Makamba amesema kuwa kutokana na athari hizi Serikali imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na taizo hili.

Serikali imeandaa mkakati wa Taifa wa kupanda na kutunza miti wa mwaka 2016-2021 ambao unalenga kupunguza kasi ya uharibifu wa ardhi kwa njia ya kupanda na kutunza miti na kuhakikisha kwamba kila mwananchi  anahusika katika utaratibu huu.

Maelekezo hayo ni pamoja na programu za upandaji miti,kuandaa mpango bora wa matumizi ya ardhi,kulima kilimo kinachofuata njia za kisasa,ufugaji bora na wa kisasa na kusisitiza matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa pamoja na kuhifadhi maji katika kipindi cha mvua.

Ametoa rai kwa wananchi wote kushiriki kikamilifu katika kutekeleza kauli mbiu  ya mwaka huu.

“Kauli mbiu ya mwaka huu ni Ardhi ni Makazi yetu Tuitunze kwa manufaa ya baadaye  hivyo wananchi wote washiriki kikamilifu katika kuitekeleza ili kuhakikisha ardhi yetu inatunzwa kwa ajili ya kizazi kijacho”,Aliongeza Makamba

Mwaka 1994 Baraza la Umoja wa Mataifa liliazimia na kuitangaza tarehe 17 mwezi juni ya kila mwaka kuwa ya maadhimisho ya siku ya kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame.Reactions:

0 comments:

Post a Comment