Thursday, 15 June 2017


NA ISMAIL NGAYONGA, MAELEZO
INAKADIRIWA kuwa takribani hekta 300,000 hadi 500,000 za Misitu nchini Tanzania inapotea kila mwaka kutokana na utumiaji wa rasilimali ya Misitu usio endelevu ikiwemo uchungaji haramu wa mifugo ndani ya Misitu ya Hifadhi, uvunaji holela wa Miti  na ufyekaji holela wa Misitu kwa ajili ya Kilimo na Makazi.
Tatizo hili si la Tanzania pekee bali ni dunia nzima hususan nchimasikini kutokana na uwezo mdogo wa Rasilimali Watu, fedha na teknolojia ya kukabiliana na maafa hayo.

Kutokana na kuongezeka kwa tatizo hili hapa nchini, Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi ya Finland imeanzisha Programu ya ’Panda Miti Kibishara’, yenye malengo ya kuwahamasisha wananchi kupanda miti kama zao la biashara.
Programu ya Panda Miti Kibiashara inatekelezwa katika wilaya sita za Ludewa, Makete, Njombe, Kilolo, Mufindi na Kilombero, na inatekelezwa kwa kipindi cha miaka 16 katika awamu nne za utekelezaji.
Lengo la Programu hiyo  ni  kuongeza kipato cha wananchi  waishio  vijijini kwa kupanda miti, kwa kuwawezesha wananchi kulima mashamba ya miti kitaalamu kwa kuzingatia matumizi  ya  mbegu bora ili mazao yatakayopatikana  yaweze kuvutia soko la ndani na nje.
Kupitia Programu hiyo imekadiriwa kuwa katika kipindi cha awamu ya kwanza ya Programu 2014-2017 jumla ya hekta 15,000 zitapandwa na wananchi waliojiunga na Vikundi vya Wakulima wa Miti.
Kwa kutambua umuhimu wa utunzaji mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii inatekeleza Mkakati wa Taifa wa Upandaji na Utunzaji Miti uliokusudia kufanya marekebisho ya changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika kampeni za upandaji miti katika vipindi mbalimbali tangu uhuru.
Akizungumza katika kilele cha siku ya mazingira duniani mwaka 2016, Waziri wa Nchi-Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba anasema  Mkakati huo wa miaka mitano (2016 hadi 2021) unakadiriwa kugharimu Tsh. Bilioni 105.2.
Amesema kuwa, masuala mengine yatakayozingatiwa katika mpango huu ni uhamasishaji na utoaji wa motisha kwa watumiaji wa nishati mbadala ili kuondoa matumizi ya kuni na mkaa.
Mhe. Makamba amefafanua kwamba, katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Upandaji na Utunzaji wa Miti, kila kijiji, kitongoji, mtaa, kaya na kila taasisi itapewa lengo la upandaji miti sambamba na kushindanisha shule na vijiji katika upandaji na ukuzaji wa miti .
“Tutarahisisha upatikanaji wa mbegu na miche. Tutashirikiana na wenzetu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, kuhakikisha kwamba Halmashauri zinatunga sheria ndogo za kulazimisha upandaji na utunzaji wa miti” anasema Makamba.
Kwa mujibu wa Makamba, anasema Serikali imekusudia kuibadilisha Tanzania kuwa ya kijani na kuendelea kuwahimiza ulimaji wa mashamba ya miti ya kibiashara kwa watu binafsi Ili kufanikisha upandaji Miti Nchini.
Katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka 15 ambao unaotekelezwa kwa vipindi vya Miaka Mitano Mitano kuanzia 2011 hadi 2025 Makamba amesema, Awamu ya kwanza ya Mpango huo (2011/2012 – 2015/2016) unasisitiza kuhifadhi wa Mazingira ikiwa ni pamoja na kupanda Miti.
Inakadiriwa kuwa Tanzania huuza wastani wa tani 12.5 za mbegu bora za miti ndani na nje ya nchi ikiwemo Msumbiji, Afrika Kusini, India, Vietnam, Guatemala, Rwanda, Uganda, Australia, Botswana, Singapore , Ufaransa, Marekani, Madagascar, Siera leone, Denmark, Costa Rica na Malawi.
Aina za mbegu zinazouzwa ni 195 na kati ya hizo, aina za miti ya kienyeji ni asilimia 60 iliyosalia ni mbegu za miti ya kigeni. Mbegu zinazoongoza kwa kupendwa katika soko ni Mkangazi, Mtiki, Mwerezi, Mkenge, Mkongo, Msindano na Mtikivuli.
Miche ya miti hiyo huzalishwa na kuuzwa kwa ajili ya matumizi ya  mbao, nguzo, mkaa, kuni, madawa, mapambo, kilimo mseto, kivuli na hifadhi ya maji, ambapo wateja wakubwa wa miti hiyo ni Idara za serikali, Makampuni binafsi, Vyama vya ushirika, Mashirika ya umma, Vyuo na taasisi za utafiti na wateja wadogo wadogo.
Ukiondoa Miti yote Duniani, hakutakuwa na maji, hakutakuwa na mvua, hakutakuwa na viumbe hai, na hakutakuwa na hewa safi, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuhamasika katika kutunza Misitu ya Asili na ile ya kuoteshwa, kupanda Miti, kuhifadhi Vyanzo vya Maji na kutunza Mazingira kwa ujumla.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment