Saturday, 6 May 2017

 Spika wa bunge Mhe. Job Ndugai

Mkurugenzi wa Itikadi,  Mawasiliano na Mambo ya Nje .
  wa CHADEMA, Mhe. John Mrema


CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)
SALAAM ZA POLE NA RAMBIRAMBI KUFUATIA AJALI ILIYOTOKEA LEO KARATU-ARUSHA  NA KUSABABISHA VIFO VYA WANAFUNZI 32 PAMOJA NA WAALIMU 2, NA DEREVA MMOJA.
Tumepokea kwa Masikitiko makubwa taarifa za ajali mbaya Iliyotokea Leo tarehe 6 Mei,2017 Mkoani Arusha, Wilaya ya Karatu na kusababisha vifo vya wanafunzi 32 (watoto wa kike 16 na watoto wa kiume 17) waliokuwa wanafunzi wa Shule ya Lucky Vincent ya Mkoani Arusha.
Aidha ajali hiyo imepoteza maisha ya watu wazima 4 ambao inasemekana ni waalimu wa Shule ya Lucky Vicent (pamoja na dereva wa gari walilokuwa wakisafiria) na kusababisha Majeruhi watoto 3 na mtu mzima 1.
Ajali hii imetokea wakati wanafunzi hawa wakiwa safarini kutokea Arusha wakienda Karatu katika ziara ya Mafunzo.
Kwa majonzi makubwa tunatoa salamu za pole kwa wazazi,  wanafunzi wa Shule ya Lucky Vicent,  uongozi wa Shule hiyo pamoja na wananchi wote wa Tanzania kwa msiba huu mkubwa na wenye kutia simanzi na huzuni kubwa.
CHADEMA tutakuwa pamoja na familia za Marehemu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo , tunawataka wanachama na watanzania wote bila kujali imani zetu tuwakumbuke wafiwa katika Sala /Dua ili Mwenyezi Mungu awatie ujasiri wafiwa katika kipindi hiki kigumu.
Aidha tunalitaka jeshi la polisi wafanye uchunguzi wa kina juu ya chanzo cha ajali hii mbaya ili matokeo ya uchunguzi huo yatumike katika kuzuia ajali nyingine kama hii kutokea siku zijazo.
Hakika taifa limepoteza watoto wake na vijana wa Kesho ambao wangelitumikia taifa letu siku zijazo.
Imetolewa Leo tarehe 6 Mei,2017  na John Mrema - Mkurugenzi wa Itikadi,  Mawasiliano na Mambo ya Nje .
Reactions:

0 comments:

Post a Comment