Wednesday, 17 May 2017Moja ya matrekta ya Kampuni ya Ursus SA ya nchini Poland likijaribiwa kuwashwa mara baada ya kuunganishwa sehemu zake na Wataalam wa kuunganisha matrekta ya Ursus kutoka Poland na Tanzania.

Majembe yatayotumika na matrekta ya Kampuni ya Ursus SA ya nchini Poland yakiwa tayari yameunganishwa na Wataalam kutoka Poland na Tanzania katika eneo la Kiwanda TAMCO lililoko Kibaha Mkoani Pwani yakiwa tayari kuanza kufanya kazi.


Wataalam wa kuunganisha matrekta ya Ursus kutoka Poland na Tanzania wakiendelea na kazi ya kuunganisha sehemu za matrekta hayo ndani ya kiwanda TAMCO lililoko Kibaha Mkoani Pwani.


Matrekta ya Kampuni ya Ursus SA ya nchini Poland yakiwa yamewekewa majembe yake tayari kwa kuanza kufanya kazi ya kulima mashambani.


Matrekta ya Kampuni ya Ursus SA ya nchini Poland yakiwa yamewekewa namba za usajili za Tanzania tayari kuanza kufanya kazi ya kulima mashambani.

 (PICHA/HABARI NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM)Mradi wa matrekta aina ya Ursus ambayo yanatengenezwa na Kampuni ya Ursus SA iliyopo nchini Poland yatawasaidia wakulima nchini kuondokana na adha ya kulima kwa kutumia jembe la mkono na kuwaongezea mazao na kipato.


Hayo yamesemwa hivi karibuni na Msimamizi wa Mradi wa Kuunganisha Matrekta hayo katika eneo la TAMCO lililopo Kibaha Mkoani Pwani, Mhandisi Adam Mbula wakati alipokutana na Waandishi wa habari na kuwaeleza shughuli zinazofanywa katika kiwanda hicho.


Mhandisi Mbula amesema kwamba, mradi huo wa matrekta ni mradi unaotokana na mkopo wa riba nafuu wa dola za Marekani milioni 55 uliotolewa na Serikali ya Poland kwa ajili ya kuisaidia Tanzania katika kukuza uchumi hususani katika sekta ya kilimo.


Amefafanua kuwa, jumla ya matrekta 2,400 yanatarajiwa kuletwa katika kiwanda hicho na kuunganishwa vipuri vyake ambapo kwa kuanzia kuna matrekta 2,004 na zana zake 200 yaani na majembe yake na jumla ya matrekta 35 yameshaunganishwa na zoezi la uunganishaji linaendelea.


Amebainisha kuwa, matrekta yanayounganishwa kiwandani hapo ni ya aina tatu yenye hosi pawa ya 50, 65, 75-85 kwakuwa kutakuwa na matrekta yenye 4x4 na 2x2 kiwandani hapo.


“Matrekta yanayokuja hapa tunayaunganisha vitu vichache tu kama vile mfumo wa umeme, mfumo wa mafuta, matairi, sehemu za kupoza injini kwakuwa tayari yameshafungwa injini na transmisheni zake, lakini baadaye kitakapojengwa kiwanda rasmi, tutakuwa tunafanya kila kitu hapa hapa na hii itaiwezesha Tanzania kujulikana”, alisema Mhandisi Mbula.


Kuhusu suala la upatikanaji wa masoko amesema kwamba, masoko yapo na tayari kuna maeneo ambayo matrekta hayo yatakuwa yakipelekwa na vituo hivyo vitakuwa vinatoa huduma ya mauzo ya matrekta na pia kuelimisha wakulima juu ya namna ya kutumia matrekta hayo ambapo ameyataja maeneo hayo ni pamoja na Morogoro, Dodoma, Njombe, Lindi, Katavi, Manyara na Nyanda za Kanda ya Ziwa ni Geita na Simiyu.


Aidha, shughuli ya uunganishaji wa matrekta hayo imeanza tangu tarehe 22 Aprili, 2017 na amesema kwamba lengo ni kuyauza matrekta hayo ambapo bei bado haijatangazwa kwakuwa kuna kitengo maalum kinachoshughulikia suala hilo na hapo baadaye itatangazwa baada ya kujua gharama zilizotumika kuyakomboa matrekta hayo, lakini pia amesema kwamba yatatolewa kwa wakulima kwa mkopo kwakuwa uwezo wao wa kuyanunua ni mdogo.


Mhandisi Mbula ameweka wazi kuwa mkopo huo unatarajiwa kurudishwa kutokana na mauzo ya matrekta hayo ambapo kwa sasa Serikali imepewa muda wa miaka mitano (grace period) ya kuanza kulipa mkopo huo.


Mradi wa Matrekta ya Ursus SA ni Mradi wenye Mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Poland katika kusaidiana katika masuala ya kiuchumi hususani kilimo na unahusisha Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC).
Reactions:

0 comments:

Post a Comment