Sunday, 14 May 2017

kaz1
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala “ Mabodi”  na kushoto ni Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Nd. Abdulghafar Idrissa akifanya kazi ya kukandika udongo katika nyumba ya mwananchi Bi. Asha Abdalla  wa Shehia ya Fuoni Migombani  aliyebomokewa nyumba yake kutokana na maafa ya mvua zilizonyesha juzi Unguja.
kaz2
Baadhi ya wananchi wakiwa katika harakati za ujenzi wa nyumba hiyo uko Fuoni Migombani  Unguja.
kaz3
Baadhi ya wananchi wakiwa katika harakati za ujenzi wa nyumba hiyo uko Fuoni Migombani  Unguja.
kaz4
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala “ Mabodi” akitoa shukrani zake kwa wananchi mbali mbali walioshiriki katika ujenzi huo na kuhakikisha Bi.Asha Abdalla anapata makaazi ya kuishi. Picha na Afisi Kuu CCM Zanzibar.
………………………………………………………
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
WANANCHI  visiwani vya  Zanzibar  wameshauriwa kuendeleza kwa vitendo  Utamaduni wa uzalendo wa kusaidiana wakati wa maafa mbali mbali yanayotokea nchini bila kujadili tofauti za kisiasa na kidini.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma Saadala “ Mabodi”   mara baada ya ujenzi wa nyumba ya  Balozi wa Nyumba kumi Bi. Asha Abdalla Baruti iliyobomoka kutokana na maafa ya mvua zinazonyesha nchini, huko Fuoni Migombani.
Dkt. Mabodi alisema maafa yanapotokea hayachagui sehemu ya kuathiri bali yanawakumba wananchi wote hivyo  ni muhimu wanajamii kushirikiana kwa mambo ya kijamii na kimaendeleo na kuacha siasa za utengano na chuki.
Ujenzi huo umefanyika kutokana na agizo la Naibu Katibu Mkuu huyo  alipowataka uongozi wa CCM na UVCCM Wilaya ya Dimani Unguja, kumjengea makaazi ya muda mwananchi huyo ambaye hakuwa  na sehemu ya kuishi kutokana na nyumba yake kuharibiwa na mvua zilizonyesha hivi karibuni.
Alisema hatua ya Chama hicho kutoa msaada na kushiriki katika masuala ya shughuli za kijamii kwa wananchi itakuwa ni utamaduni endelevu kwa Unguja na Pemba.
Alieleza kwamba lengo la CCM kutoa msaada wa kujenga makaazi ya dharura kwa wananchi wakati wa kipindi hichi cha maafa ni kuendeleza kwa vitendo siasa za waasisi wa vyama vya   ASP na TANU ambao walishiriki katika masuala mbali mbali ya kitaifa na kimataifa kwa lengo la kuwa karibu na wananchi waliowapa ridhaa ya uongozi.
Pia alisema wakati wa Kampeni za Uchaguzi CCM  ilikuwa ikienda kwa wananchi katika maeneo mbali mbali kuomba kura za kuiweka madarakani hivyo hata kwa kipindi cha maafa na changamoto zinazoikabili jamii ni lazima kirudi kwa wananchi kuwaunga mkono na kuwafariji kwa vitendo.
Naibu Katibu Mkuu huyo alisema CCM ya sasa Viongozi wa ngazi mbali mbali ndani ya Chama na Serikali kurudi kwa wananchi kujua changamoto zinazowakabili na kuzifanyia kazi kwa wakati ni jambo la lazima na sio la hiari.
“  Nasaha zangu kwa wananchi ni kwamba pindi yakitokea maafa hasa magfuriko tusaidiane kwanza kupitia umoja wetu katika mitaa mbali mbali tunayoishi kwa kuwahifadhi katika maeneo salama wenzetu wanaopata maafa huku tukisubiri serikali zetu zichukue hatua za kutoa misaada.”, alisema Dkt. Mabodi.

Pamoja na hayo aliwataka vijana nchini kuwa mstari wa mbele kwa kujitokeza muda wowote kusaidia masuala ya ujenzi wa miundombinu iliyoharibiwa na maafa ili nchi iweze kujivunia uwepo wa kundi hilo ambalo ndio nguvu kazi ya taifa.
Pia aliwataka viongozi wa kisiasa nchini kuondokana na mazoea ya kulalamika na kulaumu serikali hasa katika kipindi hichi cha maafa na badala yake wawe sehemu ya kuwahamasisha wafuasi wao wajitolee kuwasaidia watu waliofikwa na maafa huku serikali ikiendelea kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa kutatua tatizo hilo.
 Naye  Mwakilishi wa Jimbo la Fuoni, Mh. Yussuf  Hassan Iddi amesema jimbo hilo litaendelea kusaidia awamu kwa awamu wananchi mbali mbali waliopata maafa ili waweze kurudi katika hali yao ya kawaida.
Alisema uongozi wa jimbo hilo baadae utahakikisha unajenga nyumba ya kudumu kwa mwananchi huyo ili aweze kupata uhakika  wa makaazi yake.
Kwa upande wake Mbunge Mteule wa Bunge la Afrika Mashariki kwa tiketi ya CCM , Dkt.Abdulla Hasnuu Makame alisifu hatua zilizochukuliwa na CCM kwa kuendeleza utaratibu wa kuwafariji wananchi wakati wa matatizo mbali mbali ya kitaifa .
 Aliahidi kuiwakilisha vyema CCM katika Bunge hilo ili fursa mbali mbali zinazopatikana ziweze kusaidia katika kuimarisha miradi ya kijamii hasa kuongeza miundombinu ya barabara, Elimu, Afya na ajira kwa vijana.
Mapema Bi. Asha Abdalla ameishukru CCM na wananchi wote walioshiriki katika zoezi la kumjengea nyumba yake na kuongeza kwamba hatua hiyo imemfariji na kumpa nguvu za kuendelea kufanya kazi za kujipatia kipato kwa ufanisi zaidi.
Reactions:

0 comments:

Post a Comment