Tuesday, 18 April 2017SEKESEKE la Uingereza kujitoa Umoja wa Ulaya, limemsukuma Waziri Mkuu wa nchi hiyo Bi. Theresa May, kuitisha uchaguzi wa mapema, Juni 8, 2017. Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo, ulikuwa ufanyika mwaka 2020.
Bi. May ameyasema hayo leo Aprili 18, 2017 katika hotuba yake iliyorushwa Mubashara na vyombo vya habari vya kimataifa kutoka ofisini kwake 10 Downing Street jijini London.
Ametangaza uamuzi huo baada ya majadiliano ya mara kwa mara na wasaidizi wake waandamizi. 
Amesema njia pekee ya kuleta utengamano miongoni mwa Waingereza ni kufanya uchaguzi wa mapema Juni 8, 2017.
Amesema Jumatano, Aprili 19, 2017, Bunge litapiga kura kuamua kama uchaguzi huo utafanyika kama alivyopanga au la. Kwa mujibu wa taratibu za maamuzi ya bunge la Uingereza, itahitajika theluthi mbili ya wabunge ili kupitisha pendekezo lake la kufanyika uchaguzi huo wa mapema.
Kumekuwepo na kutoelewana baina ya wanasiasa wa nchi hiyo ndani ya bunge kuhusu uamuzi wa Uingereza kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya (EU), ambapo Serikali ya Bi. May imekuwa ikisisitiza kuwa uamuzi huo uliofikiwa na wananchi ni sharti upate baraka za bunge la nchi hiyo, kwa wabunge kuunga mkono uamuzi huo wa wananchi, lakini hali ndani ya bunge hilo lenye idadi kubwa ya wabunge kutoka chama cha upinzani cha Labour umekuwa ni tofauti.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment