Tuesday, 18 April 2017


NA FRANK SHIJA – MAELEZO.
KATIBU Mkuu wa wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo,(pichani juu) ameitaka kampuni ya Usambazaji wa Maji Dar es Salaam (DAWASCO) pamoja na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA), kusitisha huduma kwa wateja ambao ni wadaiwa sugu.
“Agizo la Muheshimiwa Rais, la kutaka wasiolipa bili za umeme wakatiwe huduma halimaanishi ni umeme tu bali pia hata huduma hii ya maji, kwa hivyo naagiza wale wote ambao hawataki kulipa bili za maji nao wakatiwe huduma hii, kwani hatuwezi kutoa huduma kama watu hawataki kulipa bili.” Aliagiza Profesa Mkumbo, wakati akiongea kwa mara ya kwanza na watendaji wa kampuni hizo jijini Dar es Salaam leo Aprili 18, 2017.
Profesa Mkumbo pia amesema, sambamba na hatua hiyo kampuni hizo zimetakiwa  kuongeza kasi ya utoaji huduma za maji kwa wananchi ili kufikia malengo ya Serikali katika kuwatumikia wananchi wake.
Wananchi hawataki kujua takwimu za kiasi cha maji mlicho nacho hiyo ni siri yetu, wanachotaka kukiona ni maji yanatiririka kwenye mabomba yao.” Alisisitiza.
Profesa Kitila amesema kuwa licha ya ongezeko la upatikanaji wa maji, ipo changamoto ya idadi kubwa ya wananchi kutofikiwa na huduma hivyo hivyo ni lazima sasa Mamlaka husika kuongeza kasi ya usambazaji wa miundombinu ya maji katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa.
“Pamoja na kazi nzuri mnayofanya ya kuhakikisha upatikanaji wa maji hakikisheni mnaongeza kasi ya usambazaji wa huduma hii muhimu kwa wananchi, kwakufanya hivyo mtakuwa mnatendea haki dhana ya kuwa mnaongoza kwa mapato lakini pia mnatoa huduma stahiki kwa wananchi,” alisema Profesa Kitila.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Usambazaji wa Maji Dar es Salaam (DAWASCO) Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema kuwa katika kuhakikisha uzalishaji wa maji umeongezeka kwa kutoka lita za ujazo wa mita 160 Milioni kwa siku hadi kufikia lita za ujazo mita 271Milioni kwa siku ambazo ni sawa na asilimia 100.37% ya lengo la upatikanaji wa maji ambalo ni lita 270 Milioni kwa siku.
Mhandisi Luhemeja aliongeza kuwa jumla ya Vizimba 560 (Gati za kuuzia maji) vimeunganishwa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi ikiwa ni muendelezo wa kuongeza kasi ya usambazaji na upatikanaji wa huduma ya maji miongoni mwa jamii.
Katika hatua nyingine Afisa Mtendaji Mkuu huyo amesema kuwa katika kutekeleza agizo la Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli la kuhakikisha wanakina mama wanatua ndoo za maji kichwani Dawasco inatarajia kuanza utekelezaji wa mradi wa kuongeza usambazaji wa huduma ya maji katika eneo la takribani 1,427Km unaohusisha maeneo ya Tegeta, Mpiji hadi Bagamoyo ifikapo mwezi Julai mwaka huu ambapo tayari fedha Tsh. 117Bilioni kwa ajili ya mradi huo zimepatikana kupitia Benki ya Dunia.Mradi huo utakapokamilika unakadiriwa kuongeza idadi ya watumiaji wa maji takribani laki moja.
Katika kuhakikisha inafikia azma ya kuongeza kasi ya usambazaji wa huduma ya maji kwa wananchi Dawasco inaendesha Kampeni ijulikanayo “Mama Tua Ndoo ya Maji Kichwani Ndani ya Siku 90” ikiwa na lengo la kuwaunganisha na huduma ya maji wateja takribani 151,000 wataunganishwa na huduma hiyo katika eneo linalopakana na Barabara ya Morogoro. Kampeni hiyo imeanza kuanzia tarehe 1 Aprili hadi 30 Juni, 2017.


Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji taka Jijini Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Archad Mutalemwa (kulia) akifafanua jambo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Prof. Kitila Mkumbo (kushoto) wakati Katibu Mkuu alipokutana na watedaji wa Kampuni ya Usambazaji Maji Jijini Dar es Salaam (DAWASCO) pamoja na watumishi wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji taka Jijini Dar es Salaam (DAWASA), katikati ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Usambazaji Maji Jijini Dar es Salaam (DAWASCO) Mhandisi Cyprian Luhemeja.


Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Usambazaji Maji Jijini Dar es Salaam (DAWASCO) Mhandisi Cyprian Luhemeja (kushoto) akimkaribisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Prof. Kitila Mkumbo wakati alipotembelea kampuni hiyo mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
.(PICHA ZOTE NA ELIPHACE MARWA – MAELEZO)
Reactions:

0 comments:

Post a Comment