Thursday, 13 April 2017NA ISMAIL NGAYONGA;MAELEZO
SEKTA ya Viwanda ni miongoni mwa maeneo manne ya kipaumbele yaliyoanishwa katika Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano wa 2016/17-2020/21. Maeneo mengine ni miradi mikubwa ya kielelezo, miradi wezeshi na Mawasiliano.
Mchango wa Sekta ya Viwanda katika kuendeleza uchumi uko wazi kwa kuwa nyenzo muhimu zinazosaidia shughuli za uzalishaji, usindikaji, usambazaji na masoko kwa jumla zinaratibiwa na sekta hii.
Taarifa ya Serikali inaonyesha kuwa hadi kufikia Desemba 2016, Tanzania imefanikiwa kuanzisha jumla ya viwanda 54,422 ambapo viwanda vipya 1845 viliweza kujengwa katika kipindi cha mwaka mmoja wa Utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Takwimu hizo za matokeo ya sensa ya viwanda ya mwaka 2013/14 pia zinaonyesha hadi kufikia mwaka 2013 Tanzania ilikuwa na jumla ya viwanda 49,243 ambapo viwanda vidogo vinavyoajiri mtu mmoja hadi wanne vilikuwa ni asilimia 85.13.
Aidha viwanda vidogo vyenye watu watano hadi 49 vilikuwa asilimia 14.02, wakati viwanda vya kati vyenye watu 50 hadi 90 vilikuwa asilimia 0.35 na viwanda vikubwa vyenye watu kuanzia 100 na kuendelea ni asilimia 0.5.
Kulingana na utafiti wa shughuli za Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo ya Mwaka 2012, Sekta ya viwanda inatoa ajira za moja kwa moja kwa Watanzania milioni 5.2 na kuchangia takribani asilimia 28 katika Pato la Taifa.
Malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuwa na uchumi unaoongozwa na maendeleo ya viwanda ifikapo mwaka 2025, hivyo kutekeleza adhma hiyo, nishati ni umeme inaelezwa ni nyenzo muhimu katika kutekeleza malengo hayo.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Sekta ya Viwanda ya ukanda wa Afrika Mashariki ya Mwaka 2015, umeme usiotosha ni miongoni mwa changamoto kubwa za kimiundombinu zilizopo Tanzania na nchi nyinginezo za Afrika Mashariki.
Ripoti hiyo pia inaonesha kuwa ukanda wa Mashariki wa Afrika ndio una kiwango kidogo kabisa cha uzalishaji wa nishati na wadau wanasema kukatika ovyo kwa umeme pamoja na kuwepo kwa mitambo ghali ya kuzalishia ndiyo vitu vinavyoongeza gharama.
Kwa kutambua umuhimu wa sekta ya nishati ya umeme katika maendeleo ya viwanda, Wizara ya Nishati Madini imetenga asilimia 94 ya bajeti yake  ya mwaka 2016/17 katika miradi ya maendeleo, ambapo asilimia 98 ya bajeti katika Idara ya Nishati imeelekezwa katika miradi ya umeme.
Akizungumza na Watendaji wa Benki ya Dunia hivi karibuni Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo anasema Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa  sekta ya nishati inakuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi  na kuifanya Tanzania kufikia katika kundi la nchi  zenye kipato cha kati ifikapo mwaka  2025.
Waziri Muhongo alisema  kuwa ili kuimarisha   Sekta ya Nishati,  Wizara imepanga kupanua sekta ya nishati kwa kukaribisha wawekezaji binafsi kuwekeza  katika sekta ya uzalishaji na uuzaji wa umeme pamoja na kuwapo kwa mwongozo utakaowawezesha kuzalisha umeme.
Anaongeza kuwa  Wizara inatarajia kuimarisha  usambazaji wa umeme vijijini kwa kushirikiana na  Wakala wa Nishati  Vijijini (REA) na TANESCO kupitia miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa usambazaji wa umeme  wenye msongo wa kilovolti  400 kupitia  Iringa, Mbeya, Tunduma hadi katika eneo la Kabwe nchini  Zambia.
Aliendelea kutaja miradi mingine kuwa ni pamoja na mradi wa usambazaji  umeme kupitia Mbeya, Sumbawanga, Mpanda, Kigoma, Nyakanazi na kuiomba  Benki ya Dunia kushirikiana na Benki ya Maendeleo  Afrika (AfDB) ili kufanikisha mradi huo.
Akiwasilisha Makadirio ya Hotuba ya Bajeti ya Mapato na Matumizi Wizara yake ya mwaka 2016/17, Profesa Muhongo anasema Serikali imeongeza uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini kutoka  kutoka MW 1,226.24 mwezi Aprili, 2015 hadi MW 1,461.69 mwezi Aprili, 2016 sawa na ongezeko la asilimia 19.
Anasema ongezeko hilo limechangiwa na mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia Gesi Asilia baada ya kukamilika kwa Bomba la kusafirisha Gesi Asilia kutoka Mtwara na Lindi hadi Dar es Salaam.
“Kati ya uwezo huo, MW 711.00 (asilimia 49) ni Gesi Asilia, MW 566.79 (asilimia 39) zinatokana na umeme wa nguvu za maji na MW 183.90 (asilimia 12) ni mafuta na tungamotaka. Aidha, mahitaji ya juu ya umeme yameongezeka kutoka MW 988.27 mwezi Desemba, 2015 hadi kufikia MW 1,026.02 mwezi Machi, 2016 sawa na ongezeko la asilimia 4.15” anasema Prof Muhongo.
Kwa mujibu wa Profesa Muhongo anasema kiasi cha umeme kilichoingizwa kwenye Gridi ya Taifa kiliongezeka kutoka GWh 6,033.98 Mwaka 2014 na kufikia GWh 6,227 Mwaka 2015, sawa na ongezeko la takriban asilimia 3.
Aidha Prof. Muhongo anasema kiwango cha upatikanaji wa huduma ya umeme  kimekuwa kikiongezeka mwaka hadi mwaka, ambapo Watanzania waliofikiwa na huduma hiyo wameongezeka kutoka asilimia 36 mwezi Machi, 2015 hadi kufikia takriban asilimia 40 mweziAprili, 2016.
Sekta ya Viwanda ndiyo hasa inayoshikilia ufunguo wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini kutokana na uwezo wake wa kutengeneza ajira na kubadilisha maisha ya Watanzania.
Ni wajibu wa  sekta ya umma na binafsi kufanya kazi kwa pamoja katika misingi ya uzalendo ili kuchambua changamoto mbalimbali zilizopo katika sekta ya viwanda na hivyo kupata suluhishi la kudumu.
Reactions:

0 comments:

Post a Comment