Monday, 24 April 2017

 NA DAUDI MANONGI-MAELEZO.

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto imeanza hatua za awali za uainishaji wa gharama,uandaaji wa mfumo mbadala na upembuzi wa kina wa aina ya ubia ili kushirikiana na Sekta binafsi katika utoaji wa huduma za uchunguzi wa magonjwa.
Hayo yamesemwa leo bungeni na Naibu Waziri, Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe.Hamis Kigwangalla wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge Mjini Dodoma.
“Kufuatia kukua kwa kasi kwa Sayansi na Teknolojia ya uchunguzi wa magonjwa,Wizara inakubaliana na wazo hili juu ya kuangalia namna nzuri ya kushirikiana na sekta binafsi katika utoaji wa huduma hizi,”Alisema Mhe.Kigwangalla.
Amesema kwa kuanzia sasa Wizara yake inafikiria kuanzisha ushirikiano kwa kupitia ukodishaji wa vifaa ambapo Serikali itakodisha mashine hizo ambazo zitakuwa za mbia na Serikali haitahusika na ununuzi,ufungaji na matengenezo kinga ya mashine hizo.
Aidha amebainisha kuwa katika mfumo huo,Wizara itakuwa na jukumu la kusimamia utoaji wa huduma na itapata gawio lake kutokana na makusanyo yatokanayo na uchangiaji wa huduma kulingana na mkataba.
“Ni imani ya Wizara kuwa kutumia mfumo wa ubia na sekta binafsi(PPP) huduma za uchunguzi wa magonjwa zitaimarika na kuipunguzia Serikali mzigo wa gharama”,Aliongeza Mhe.Kigwangalla.

SERIKALI YAONDOA TOZO ZISIZO ZA LAZIMA KATIKA ZAO LA KOROSHO
SERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo,Mifugo na Uvivu imesema imeshughulikia malalamiko  ya wakulima wa Korosho kwa kuondoa makato yasiyokuwa muhimu katika zao hilo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Wizara hiyo Mhe.William Ole Nasha wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge leo Mjini Dodoma.
“Serikali imekwisha fanyia marekebisho maeneo ambayo wakulima walikuwa wanalalamikia kwa kuondoa kabisa makato hayo katika zao hilo”, Aliongeza Mhe.Ole Nasha.
Amesema kuwa Serikali imefuta ushuru wa shilingi 20 kwa kilo kwa ajili ya chama kikuu cha Ushirika,Shilingi 50 za usafirishaji wa Korosho,Shilingi 10 kwa kilo ajili ya mtunza ghala na pia shilingi 10 kwa kilo kwa ajili ya kikosi kazi cha Masoko.Aidha Sekta ina utaratibu maalum wa kupanga bei dira kwa kutumia vigezo vinavyokubaliwa kwa pamoja na wadau wote.
Kwa upande wa manunuzi ya pembejeo za korosho amesema hufanywa kwa pamoja na vyombo rasmi ndani ya Tasnia ambapo awali ilikuwa ikisimamiwa na mfuko wa Maendeleo ya Korosho na sasa Bodi ya korosho Tanzania.
Aidha ameeleza changamoto zinazojitokeza katika kufikisha pembejeo hizo kwa wakulima wa korosho na hatua zimechukuliwa kwa kushirikisha vyama vya ushirika ili kudhibiti mianya ya pembejeo kwenda kwa wasio lengwa.

Pia Serikali imeweka mfumo wa usambazaji wa pembejeo wenye lengo la kuhakikisha kwamba pembejeo hizo zinawafikia walengwa pekee.
“Utaratibu huu unazingatia kutambua wakulima wenye uhitaji na pembejeo na hununuliwa kwa kutumia utaratibu wa ununuzi wa pamoja n akusambazwa kwa wakulima kwa kutumia wakala  walioteuliwa na kudhibitishwa na Halmashauri husika”,Alisisitiza Mhe.Ole Nasha.

Mwenyekiti  wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mussa Azzan Zungu akiongoza kikao cha kumi na moja cha Mkutano wa saba wa Bunge la 11 leo Mjini Dodoma Aprili 24, 2017.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. George Simbachawene akijibu maswali mbalimbali ya wabunge katika kikao cha kumi na moja cha Mkutano wa saba wa Bunge la 11 leo Mjini Dodoma Aprili 24, 2017.


Naibu Waziri wa Ujenzi uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Edwin Nyonyani akijibu maswali mbalimbali ya wabunge katika  kikao cha kumi na moja cha Mkutano wa saba wa Bunge la 11 leo Mjini Dodoma Aprili 24, 2017.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment