Thursday, 20 April 2017

  DSC_6566  
  HUSNA SAIDI NA JACQUILINE MRISHO – MAELEZO.
 
Kampuni ya Harusi Trade Fair imejipanga kukutanisha wafanyabiashara na watoa huduma wa bidhaa za harusi ili waweze kufahamiana na kuonesha bidhaa zao.
 
Meneja Biashara wa Kampuni hiyo, Hamis Omary ameyabainisha hayo leo Jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maonesho ya Harusi Trade Fair yanayotarajia kufanyika Mei 12 hadi 13 mwaka huu katika ukumbi wa Golden Tulip.
 
Omary alisema maonesho hayo ya tisa ya bidhaa na huduma za harusi ni moja ya maonesho makubwa  ambayo hufanyika mara moja au mbili kila mwaka na yanashirikisha wadau mbalimbali kutoka nchi za Afrika Mashariki na Pwani.
 
“Tunapenda kuwatangazia wananchi kujumuika na sisi katika maonesho haya kwani ni ya kipekee, yanavutia, yanaburudisha pamoja na kurahisisha maharusi kuandaa harusi zao.Vile vile kutakuwa na mitindo mipya kutoka kwa wauzaji bora katika sekta ya harusi” alisema Omary.
 
Meneja huyo aliongeza kuwa kadri maonesho hayo yanavyoendelea kukua mwaka hadi mwaka yanazidi kuwa maonesho bora  kwani wanajifunza njia mbalimbali za kutatua changamoto zinazojitokeza katika maonesho hayo.
 
Kwa upande wake Mratibu wa maonesho hayo, Naomi Godwin alisema kuwa lengo la maonesho hayo ni kuwapa maharusi mahitaji yao muhimu hivyo ni vizuri kuona na kutumia bidhaa na huduma hizo  ili kupendezesha sherehe zao.
 
”Maonesho haya yatafanyika bure hivyo huu utakua muda mzuri kwa maharusi pamoja na familia zao kukutana na wabunifu mbalimbali watakaowabunia sherehe zinazoendana na wakati”alisema Naomi.
 
Nae Meneja Msaidizi kutoka Golden Tulip Hotel, Adele Johnson amesema kuwa wameamua kudhamini maonesho hayo ili kuwavutia wananchi wengi kufika katika eneo hilo.
 
Maonesho hayo yanatarajiwa kuhudhuriwa na wafanyabiashara zaidi ya 30 wanaohusika na huduma za harusi wakiwemo wapiga picha, huduma za vyakula,wapambaji ukumbi,huduma za nywele, wapamba nyuso, pamoja na wamiliki wa kumbi za sherehe.
Reactions:

0 comments:

Post a Comment