Friday, 28 April 2017NA HUSNA SAIDI- MAELEZO
CHAMA cha Kutetea Abiria Tanzania (CHAKUA) kimeishauri Serikali kuanzisha mfumo wa kukata tiketi kwa njia ya mtandao ili kudhibiti tiketi feki zinazotolewa na baadhi ya mabasi yaendayo mikoani katika stendi  kuu ya mabasi ya Ubungo, Jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti Taifa wa CHAKUA, Hassan Mchanjama alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu utoaji wa tiketi feki kwa mabasi yaendayo mikoani, leo Jijini Dar es Salaam
Mchanjama alisema kuwa, Aprili 21 mwaka huu  chama hicho kiliiandikia  barua Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yenye kumbukumbu namba CHAKUA/KMN/04/2017 kuiomba Serikali kuanzishA mfumo mpya wa ukataji tiketi kwa njia ya mtandao ili kuepukana na ubababishaji, utapeli na wizi wa kila siku unaofanywa na baadhi ya Mawakala, Makarani na wapiga debe katika stendi zote nchini Tanzania.
“Kumekuwa na wimbi kubwa la tiketi feki ambazo hutolewa na mawakala wa mabasi katika stendi ya mabasi ya Ubungo na Mbeya, hiyo ni kutokana na kukamatwa kwa baadhi ya vitabu vya tiketi ambavyo vimefojiwa TIN namba bila kibali kutoka TRA”, alisema Mchanjama.
Aliongeza kwa kusema, mfumo huo wa ukataji wa tiketi kwa njia ya mtandao utasaidia kuokoa muda, kuondoa kero za abiria kuibiwa, kuwabana Mawakala na Makarani ambao wamakuwa wakitoroka na mauzo ya tiketi, wamiliki kupata pesa zao kwa uhakika, kujua idadi kamili ya abiria waliokuwepo ndani ya basi husika, kujua idadi ya watu waliopoteza maisha na majeruhi pindi ajali zinapotokea pamoja na kusaidia Serikali kukusanya kodi kwa urahisi na uhakika.
Aidha, CHAKUA imefanya utafiti kwa muda mrefu na imegundua njia pekee ya kuondoa matatizo hayo ni kuhama katika mfumo unaotumika sasa na kuingia kwenye mfumo wa mtandao (ki-electronic) ambao una mafanikio na ufanisi mkubwa hususani unaotumika katika mabasi ya mwendokasi UDART (BRT).
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki na Katibu wa Marine, Wilson Sylvester Damo aliwataka abiria kuwa na mazoea ya kukata tiketi kwenye sehemu husika zinazojulikana kisheria ili kuepukana na usumbufu unaojitokeza.
Nae, Katibu Idara ya Reli Maulid Masalu aliwataka waandishi wa habari kushirikiana kwa ukaribu na CHAKUA kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na faida ya utumiaji wa mfumo wa kukata tiketi kwa njia ya mtandao kwani ni salama zaidi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment