Monday, 6 March 2017

Tundu Lissu, akiwa ameketi sanjari na polisi wa mahakama ya hakimu mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, leo Machi 17, 2017 muda mfupi kabla ya kufutiwa mashtaka na serikali na kukamatwa tena na polisi
MWANASHERIA Mkuu wa CHADEMA, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, amefutiwa mashtaka ya uchochezi, baada ya Ofisi ya mashtaka ya serikali kuieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, leo Machi 6, 2017 kuwa haina haja ya kuendelea na kesi hiyo ya uchochezi.

Hata hivyo Mwanasheria huyo machachari, alikamatwa hata kabla ya kuondoka kwenye mahakama hiyo na sasa anashikiliwa kwenye kituo kikuu cha polisi jijini Dar es Salaam.
Habari za kukamatwa kwake amethibitisha Tundu Lissu mwenyewe  kwenye ukurasa wake wa Facebook, akiuarifu umma wa Watanzania.
“Nimekamatwa tena hapa hapa mahakamani Kisutu mara tu baada ya waendesha mashtaka wa serikali kunifutia kesi iliyotokana na kukamatwa kwangu bungeni Dodoma mwezi uliopita.”. Ameandika Tundu Lissu.
Amesema serikali imeifuta kesi hiyo kwa maelezo kwamba haina nia tena ya kuendelea na kesi hiyo. “Sikutoka hata nje ya mahakama nikakamatwa tena. Wamenileta Central kwa mahojiano. Mapolisi walionikamata wamekataa kuniambia wananikamata kwa kosa gani.” Ameendelea kuandika Tundu Lissu ambaye anagombea Urais kwenye uchaguzi Mkuu wa chama cha Wanasheria Tanzania, (TLS), utakaofanyika wiki ijayo jijini Arusha.
Tundu Lissu katika maelezo yake amesema “Nadhani sababu ina uhusiano wa moja kwa moja na Uchaguzi wa Rais wa TLS unaofanyika wiki ijayo. Serikali hii, kwa kutumia mawakili wao, imekuwa na mkakati mkubwa wa kunizuia kugombea urais wa TLS.” Amesema Mwanasheria huyo.
 
Reactions:

0 comments:

Post a Comment