Thursday, 16 March 2017MTOTO wa Rais staafu wa awamu ya Nne, Ridhiwani Kikwete amekiri kuitwa na Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za kulevya na kuhojiwa.
Ridhiwani ambaye pia ni mbunge wa Chalinze mkoani Pwani alisema mahojiano hayo yalikuwa chini ya Kamishna wa Mamlaka hiyo, Rogers Sianga.
Akihojiwa leo Machi 17, 2017 na televisheni ya Azam TV, kwenye taarifa yake ya habari ya saa mbili usiku, Ridhiwani alisema imekua ni faraja kubwa kwake kuitwa na kuhojiwa kwani kumekuwepo na habari nyingi zinazosambazwa na vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii ikimuhusisha yeye na biashara hiyo.
“Huu ulikuwa ni wakati mzuri wa kuondoa tetesi zilizokuwepo kwa muda mrefu na ilifikia wakati niliwahi kitwa na mzee wangu (Rais Kikwete), na kuniuliza kama ni kweli habari zinazozagaa zinaukweli wowote, nilimueleza kuwa si za kweli na wala sihusiki na biashara hivyo.”
Kuhusu mahojiano hayo, Ridhiwani hakuingia kwa undani zaidi bali akijibu swali la mtangazaji wa Azam TV, Charles Hillary, kuwa nini matokeo ya mahojiano hayo na kama atatakiwa kurudi tena. “Baada ya kuhijiwa sikuambiwa kitu chochote na niliruhusiwa kuondoka.” Alisema.
Kwa muda mrefu sasa kumekuwepo taarifa kuwa mtoto huyo wa Rais mstaafu alikuwa akishiriki biashara hiyo haramu hali iliyopelekea kuwepo na shinikizo kuwa na yeye akamatwe na kuhojiwa.
Reactions:

0 comments:

Post a Comment