Wednesday, 22 March 2017


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye akikabidhiwa ripoti ya uchunguzi kuhusu tuhuma za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kuvamia Kituo cha Televisheni cha Clouds Media na Mwenyekiti wa Kamati ya uchunguzi wa sakata hilo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO, Dkt. Hassan Abbass leo Jijini Dar es Salaam.


Mwenyekiti wa Kamati ya uchunguzi wa tuhuma za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kuvamia kituo cha Televisheni cha Clouds Media ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO, Dkt. Hassan Abbass (kushoto) akimwelezea Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye ushahidi wa CCTV uliombatanishwa katika CD aliyomkabidhi leo Jijini Dar es Salaam.


NA K-VIS BLOG
NA K-VIS BLOG
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, amepokea ripoti ya kamati ya masaa 24 aliyoiunda kuchunguza kiini cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, “kuvamia” studio za Clouds Media Group jijini Dar es Salaam, akiwa na askari waliobeba bunduki, usiku wa Machi 17, 2017.
Waziri Nape alipokea taarifa hiyo leo Machi 22, 2017 jijini Dar es Salaam, hata hivyo ikiwa imechelewa sana kutokana na agizo lake kuwa ifanye kazi kwa saa 24 tangu alipoiunda Jumatatu Machi 20, 2017.
Taarifa hiyo ilikabidhiwa kwake na Mwenyekiti wake, Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo ambaye pia ndio Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo alieleza sababu za kuchelewa kuwasilishwa kwa ripoti hiyo ilitokana na mtuhumiwa (Mkuu wa Mkoa), kutopatikana hadi ripoti hiyo inawasilishwa.
Akizungumza kabla ya kwuasilisha ripoti hiyo, Mjumbe wa Kamati, Deodatus Balile alisema, kamati yake iliwahoji jumla ya wafanyaakzi 14 wa Clouds Media Group na licha ya jitihada za kumtafuta Mkuu wa Mkoa Paul Makonda, kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kumfuata ofisini kwake hawakufanikiwa kumuona.
“Tulimpigia simu mara kadhaa lakini hakupokea.” Alisema Balile na kuongeza, "Hata tulipofika katika ofisi yake, aliondoka kupitia mlango wa nyuma.” Alibainisha Balile.
Alisema baada ya jitihada hizo zote kugonga mwamba, kamati yake ilijiridhisha kuwa Mkuu wa Mkoa amechagua mwenyewe kutoitumia fursa ya kuhojiwa na kamati ili kupata maelezo ya upande wake.
"Katika uchunguzi wetu, tumejiridhisha kuwa Mkuu wa Mkoa alivamia kituo cha Clouds akiwa anaendesha gari mwenyewe na akiwa na askari wenye silaha na waliingia ndani ya studio iliyokuwa ikipeperusha matangazo.” Alifafanua Balile
Pia Babile alisema Kamati ilijiridhisha pia kuwa palikuwa na vitisho dhidi ya walinzi na wafanyakazi kwa kutumia askari hao waliobeba silaha za moto.
"Miongoni mwa vitisho ni kuwalazimisha kurusha kipindi vinginevyo angewaingiza kwenye tuhuma za dawa za kulevya au kuwafunga jela miezi sita". Alifafanua Mjumbe huyo wa Kamati.
Aidha Balile alisema kamati ilijiridhisha pia, Mkuu wa Mkoa Makonda, aliingilia taratibu za uhariri kwa kulazimisha habari anayotaka irushwe hewani kinyume na utaratibu na maadili ya uandishi wa habari.
"Kamati haikuona uthibitisho wowote kuwa kuna wafanyakazi waliopigwa na vitako vya bunduki au kupigwa mitama" , alisema
Aidha kamati imekuja na mapendekezo matatu ambayo ni pamoja na
1)  Mkuu wa mkoa aombe radhi Clouds na kwa wanahabari wote.
2)  Waziri husika atoe taarifa kwa mamlaka husika ili Mkuu wa Mkoa achukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria.
3)  vyombo vya usalama kufanya uchunguzi juu ya askari kuingia Clouds na silaha za moto.

Kwa upande wake Waziri Nape alisema, aliipongeza kamati hiyo kwa kukamilisha kazi hiyo ngumu na bila malipo na kazi yake ni kuipeleka ripoti hiyo kwa wakuu wake, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu. “Nikiri kwamba sisi ni binadamu, tunaweza kuwa na madhaifu ya hapa na pale, na inapotokea tatizo ni vizuri kujifunza kuwa mnyenyekevu kwani unalipwa na kodi za wananchi na ukiwa mnyenyekevu ni Baraka kwa Mwenyezimungu.” Alisema Nape.

Katibu wa Kamati ya Kuchunguza Sakata la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuvamia ofisi za Kituo cha Televisheni cha Clouds Media, Deodatus Balile akielezea yaliyomo katika ripoti yao kabla ya kumkabidhi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Moses Nauye (kushoto) leo Jijini Dar es Salaam.Reactions:

0 comments:

Post a Comment