Thursday, 2 March 2017NA K-VIS BLOG
MWANDISHI mkongwe na Mwanasheria, Jenerali Ulimwengu, leo Machi 2, 2017, ameonekana Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, akiwa kwenye jopo la mawakili wanaomtetea Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, katika kesi Katiba aliyofungua kwenye  mahakama hiyo akimlalamikia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Kanda hiyo, Camilius Wambura.
Ulimwengu, ameungana na jopo la mawakili, Tundu Lissu, Peter Kibatala na John Malya katika kumtetea Mbowe.
Aidha katika kesi hiyo leo hii, Mahakama, imetupilia mbali maombi yaliyowasilishwa na Mbowe ya kutaka asikamatwe hadi kesi yake ya msingi, itakapomalizika.
Maombi hayo yalitupwa kwa sababu kifungu cha sheria kilichotumika kuyafungua si sahihi na kwamba hutumika pale ambapo sheria ziko kimya.
Uamuzi huo wa majaji umefikiwa kutokana na pingamizi la Jamhuri lililowasilishwa na wakili mkuu wa serikali, Gabriel Malata kuiomba kuyatupilia mbali maombi hayo kwani hayana msingi kisheria.
Mbowe amefungua kesi hiyo ya kikatiba namba 1, ya mwaka 2017 dhidi ya wadaiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam na Ofisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu ya Dar es Salaam. Kesi hiyo itasikilizwa tena Machi 8, mwaka huu. Pichani juu, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, (kushoto), akitafakari jambo ndani ya Mahakama kuu kanda ya Dar es Salaam akiwa na wakili wake Jenarali Ulimwengu (katikati) na Meya wa Ubungo Boniface Jacob leo Machi 2, 2017.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment