Thursday, 16 March 2017


K-VIS BLOG NA MASHIRIKA YA HABARI
HATIMAYE Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF), aliyekaa madarakani kwa muda mrefu, Mzee Issa Hayatou,(70), pichani juu, “ameng’oka” kwenye nafasi hiyo kufuatia ushindi mnono alioupata mpinzani wake, Rais wa chama cha soka cha Madagascar, Ahmad Ahmad, kufuatia uchaguzi mkuu wa Shirikisho hilo, uliofanyika mjini Addis Ababa Ethiopia leo Machi 16, 2017.
Katika uchaguzi huo, Ahmad Ahmad alijikusanyia jumla ya kura 30 ikiwa ni kura 10 zaidi ya Hayatou aliyeambulia 20.
Matokeo hayo yanahitimisha miaka 29 ya utawala wa Hayatou kama kiongozi wa juu wa soka barani Afrika.
Hayatou alikuwa rais wa CAF tangu mwaka 1988 wakati huo Lionel Messi akiwa na miezi tisa tu tangu azaliwe wakati mtawala huyo mzaliwa wa Cameroon alipotangazwa kusimamia soka la bara la Afrika.

Wakati huo huo, kilio cha Wazanzibara kimepata jibu baada ya mkutano mkuu wa 39 wa Shirikisho la soka barani Afrika (CAF) unaoendelea mjini Addis-Ababa, Ethiopia, umepitisha ombi la chama cha soka Zanzibar (ZFA) kuwa mwanachama rasmi wa CAF.
Ni jambo la kihistoria kwa Zanzibar kwani safari hii ombi lao limepitishwa bila kupingwa na inakuwa nchi ya 55 mwanachama wa kujitemea wa CAF.
Awali Zanzibar ilikuwa inaunganishwa na Tanzania bara chini ya TFF na kupelekea kukosa haki za kushiriki kama nchi kwenye mashindano yanayoandaliwa na CAF pamoja na yale ya FIFA.
Pendekezo hilo lilipelekwa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ndugu, Jamal Malinzi na lilipokelewa na wajumbe 54 wengine waliokuwepo.
Hii maana yake ni kuwa kwa sasa CAF ndio shirikisho mwanachama wa FIFA kwa upande wa mabara lenye wanachama wengi zaidi kuliko wote.
Vilabu vya Zanzibar vimekuwa vikishiriki mashindano mbalimbali ya CAF lakini kwa ngazi ya kitaifa hawakuwa na ruhusa na walicheza kwa kuungana na Tanzania bara na kushiriki kama Tanzania.
Kwa maana hiyo basi, chama cha soka cha Zanzibar kitapata uwezeshaji wa kifedha moja kwa moja kutoka CAF na FIFA kwa ajili ya timu ya taifa.


Rais mpya wa CAF, Ahmad Ahmad
Reactions:

0 comments:

Post a Comment