Tuesday, 21 February 2017

NA K-VIS BLOG
“Pambano hili la Simba na Yanga, ningeshauri Mamlaka zinazosimamia mpira kuongeza waamuzi, wawepo waamuzi sehemu za magoli, hili linawezekana hata kwa wenzetu jambo hili hufanyika, hii itasaidia kuongeza umakini katika maamuzi ya mchezo huu.” Anasema Kipa wa zamani wa Simba na timu ya Taifa Mohammed Mwameja.
Mwameja ameyasema hayo katika kipindi cha runinga cha asubuhi cha Morning Trumpet kinachopeperushwa na Azam TV leo Februari 22, 2017 kuelekea pambano la watani wa jadi baina ya Simba na Yanga linalotarajiwa kufanyika Jumamosi hii ya Februari 25, 2017.
Mwameja ambaye alisifika sana kwa umahiri wake wa kunyaka mipira awapo langoni, na kupewa jina la Tanzania One, amesema, matokeo ya michezo ya Simba na Yanga mara nyingi haitegemei ubora wa timu, kwani wachezaji, wanachama na viongozi hutawaliwa na “tention” (mhemko) kwa hivyo ushindi kwa timu hizi hutegemea jinsi mchezaji ameamkaje siku hiyo ameandaliwa vipi kisaikolojia.
Mwameja pia ameonyesha kusikitishwa na mtindo wa sasa wa kutegemea sana wachezaji wa nje na kuwaacha wachezaji wa ndani.
“Hii kitu inaniumiza siifurahii kabisa, tutegemee wachezaji wa nje kufunga mabao ilhali tunao wachezaji wa ndani ambao tukiwaandaa vizuri wanaweza kuwa wazuri zaidi, tunachokifanya hivi sasa ni kama Uingereza, hii haina mwisho mzuri.” Alisema Mwameja
Katika kipindi hicho cha runinga kilichokuwa kikiongozwa na Patrick Nyembere, alikuwepo pia mshambuliaji hatari wa Yanga na Timu ya Taifa Makumbi Juma, (Homa ya jiji), ambaye naye kwa maoni yake, alisema, matokeo ya pambano hili la watani wa jadi huenda ikaamua nani atakuwa bingwa msimu huu.
“Makosa madogo ya pambano la Simba na Yanga, ni kama umehukumiwa.” anaonya Mwameja.
Aidha, kwa upande wake, Makumbi Juma, ameitahadharisha Yanga kuwa, isiuchukulie mchezo huo wa Jumamosi kuwa utakuwa rahisi kwao, kwani Simba ya sasa ina tofauti kubwa sana na ile ya miaka miwili iliyopita.
"Yanga wanapaswa kuwa makini na wachezaji wacheze wakiwa na malengo, na malengo ni kushinda." Alisema Makumbi.
Makumbi Juma, "Homa ya jiji"
Reactions:

0 comments:

Post a Comment