Tuesday, 21 February 2017NA K-VIS BLOG
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, leo Februari 21, 2017 imeweka zuio la muda likielekeza Mwenyekiti wa CHADEMA, na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, asikamatwe wala kuwekwa kizuizini hadi hapo kesi yake ya msingi ya kikatiba dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa kanda hiyo, (ZCO),  Camilus Wambura, itakapokamilika.
Jopo la majaji watatu, Sekieti Kihiyo ambaye ni kiongozi wa jopo hilo, akisaidiana na Jaji Lugano Mwandambo na Jaji Pellagia Kaday, wametoa uamuzi huo leo Februari 21, 2017, wakati wa kusikiliza shauri hilo kwa mara ya kwanza ambalo lililofunguliwa na Mwenyekiti wa CHADEMA na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, ambaye pamoja na mambo mengine, anapinga mamlaka ya RC kumkamata kwa kile anachokiita kudhalilisha watu.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama Kuu ya Tanzania baada ya kesi hiyo kuahirishwa, Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu, alisema,
Mteja wake (Mbowe), anaiomba mahakama hiyo itamke kuwa vifungu vya Sheria ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa vinavyowapa mamlaka wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuwakamata watu na kuwatia mbaroni viko kinyume cha Katiba.
“Uamusi wa kwanza unahusu maombi ambayo tuliyawasilisha mahakamani ya kuomba hao wanaotaka kumkamata mwenyekiti wazuiwe na mahakama hadi hapo shauri la msingi tulilolifungua yatakaposikiklizwa hadi hapo Ijumaa, Mahakama imesema kwamba polisi wanaweza kumuita kwa mahojiano lakini sio kumkamata na pia Mahakama imeridhia kufanya marekebisho kwa kumuingiza Mwanasheria Mkuu wa serikali.” Alisema Tundu Lissu.
Mapema mwezi huu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alimtaja Mbowe na watu wengine kadhaa kiwemo Mfanyabiashara Yusuf Manji, na Askofu Josephat Gwajima kuwa ni miongoni mwa watu 65, walio katika orodha ya pili ya watu wanaotuhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya.
Wakati Mbowe, aliitisha mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma, alikanusha vikali kujihusisha na dawa za kulevya na kueleza masikitiko yake ya kudhalilishwa kwa kutajwa na kwamba anapanga kufungua kesi Mahakama Kuu ya kupinga hatua hiyo ya Mkuu wa Mkoa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment