Thursday, 5 January 2017NA DAUDI MANONGI-MAELEZO
SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu,Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi – VETA wanaendesha mpango wa kutathmini na kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya Mfumo rasmi wa Mafunzo.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Katibu Mkuu wa Kazi, Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu Eric Shitindi, imesema kuwa mpango huo unatoa fursa ya kufanyiwa tathmini ya ujuzi, kupewa mafunzo, kuziba upungufu na kisha kutunukiwa cheti.


Taarifa hiyo inaeleza kuwa sifa za mwombaji wa mafunzo hayo ni pamoja na uzoefu usiopungua miaka mitano na umri usiozidi miaka 45.

Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa fani mbalimbali zitakazohusika ni Uashi, Useremala, Ufundi Magari (makenika), upishi, uhudumu wa hoteli, Bar na Migahawa.

Ili kufanya maombi waombaji wanatakiwa kufika katika ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa, Mji au Wilaya iliyoko karibu ili kuchukua fomu za kujaza maombi bila malipo yeyote na maombi hayo kuwasilishwa kuanzia tarehe 5 hadi 25 Januari 2017.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa mchakato wote wa tathmini na urasimishaji wa ujuzi utagharamiwa na Serikali na pia watakaokidhi sifa, vigezo na masharti watajulishwa kwa ajili ya usaili kuanzia Tarehe 10 Februari 2017.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment