Tuesday, 31 January 2017

Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt.Harrison Mwakyembe.

Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo, Mjini Dodoma limepisha Muswada wa Sheria ya Huduma ya Msaada wa Kisheria wa Mwaka 2016 (The Legal Aid Bill, 2016).

Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe alipokuwa akitoa taarifa wakati wa kuwasilisha muswada huo amesema kuwa muswada huo wa sheria umepitia hatua nyingi na umechukua muda mrefu hadi kufikia hatua ya kujadiliwa na Bunge tukufu.

Aliendelea kwa kusema kuwa muswada huo unapendekeza kutungwa kwa sheria ya msaada wa kisheria kwa lengo la kuanzisha (kwa mara ya kwanza katika histori ya nchi) mfumo wa kisheria wa kusimamia, kuratibu, kurasimisha na kutambua utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria katika mashauri yote ya Jinai na Madai kwa mahitaji.

Aidha utaratibu uliokuwepo kwa miaka mingi kwa upande wa Serikali unahusu baadhi tu ya makosa ya Jina, makosa yenye adhabu kubwa kama vile ya kunyongwa hadi kufa na vifungo virefu. Ambapo huduma hiyo imekuwa ikitolewa katika ngazi ya Mahakama Kuu pekee na kwa wigo mdogo tu pale inapohitajika kwa maslahi ya haki na kwa maelekezo ya Jaji Mkuu au yeyote aliyekasimiwa mamlaka ya kutoa maelekezo hayo.

“Kumekuwepo na ongezeko kubwa la mahitaji ya huduma ya msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria. Kutokana na hali hiyo, Serikali imeona ulazima wa kuanzisha mfumo wa kusimamia na kuratibu utoaji wa huduma hiyo ili kuhakikisha inatolewa na watu wenye sifa, kwa wahitaji halisi na kwa taratibu zinazofahamika ili iendane na matakwa ya kikatiba,” alifafanua Dkt. Mwakyembe.

Vile vile ameeleza kuwa muswada huo unalenga kuwatambua wasaidizi wa kisheria, kufuta sheria ya msaada wa kisheria (katika mashauri ya Jinai).
Kwa upande wake Mbunge Selemani Zedi amesema kuwa, muswada huo utawasaidia wananchi ambao hawana uwezo wa kuwalipa Mawakili wanapohitaji msaada wa Kisheria.

Aidha, Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson ameipongeza Serikali kwa muswada huo muhimu ambao Bunge umeipitisha unasuobiria kutiwa saini na Mhe. Rais ili kuwa Sheria.
Reactions:

0 comments:

Post a Comment