Tuesday, 17 January 2017


NA BEATRICE LYIMO-MAELEZ0
SERIKALI imesitisha waraka wa muongozo uliotolewa kuhusu matumizi ya mihuri kwa wenyeviti wa Mitaa na vijiji mpaka pale itakaposhirikiana na kukubaliana namna bora ya kuendesha masuala ya kuhudumia wananchi.
Akizungumza na baadhi ya wenyeviti wa mtaa, Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. George Simbachawene amewataka wenyeviti wa mitaa nchini kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria na taratibu zilizopo.
Mhe.Simbachawene alisema kuwa nia ya kusitisha waraka huo ni kuweka utendaji mzuri baina ya Serikali na watendaji wake wa chini.
“Utaratibu uliopo uendelee mpaka pale Serikali itakapotoa utaratibu mwingine wa matumizi mbalimbali ya mihuri hiyo baada ya kujadiliwa na kushirikiana vya kutosha” alifafanua Waziri Simbachawene
Mhe.Simbachawene alisema kuwa kuna baadhi ya wenyeviti wa mitaa wamekuwa wakitumia vibaya mihuri hiyo na kupelekea migongano na migogoro ya ardhi katika vijiji na mitaa ikiwemo maeneo ya Ununio, Temeke.
Mbali na hayo alisema kuwa katika Tangazo la Serikali namba 3 lililotolewa 5 Septemba, 1994 limeeleza baadhi ya vitendea kazi vya mwenyekiti wa mtaa ni bendera yenye nembo ya Halmashauri, daftari ya kutunza kumbukumbu na rejista ya makazi.
Alisema kuwa mamlaka ya mwenyekiti haitokani na mihuri, bali utendaji uliopo ndani ya mtaa au kijiji husika, hivyo mamlaka ya mwenyekiti ipo pale pale na haibemwi na muhuri bali muhuri huonesha nguvu ya ofisi baada ya kuwashirikisha watendaji tofauti ndani ya kijiji katika kutoa maamuzi.
“Mhuri si mali ya mwenyekiti binafsi, hivyo kwa yeyote atakayekiuka matumizi ya mihuri hiyo Sheria itachukua mkondo wake” alisisitiza Mhe. Simbachawene.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Wilaya ya Temeke Bakiri Makele, ameahidi kushirikiana na Serikali kwa kutumia mihuri hiyo kwa kufuata Sheria na taraibu zilizopo.
Naye Katibu wa Wenyeviti hao, Marium Machicha alimshukuru Waziri mwenye dhamana kwa kauli aliyoitoa baada ya kuliona tatizo hilo na kuahidi kulifanyia kazi.
Serikali ilitoa Muongozo huo wa namna wa matumizi ya mihuri kwa wenyeviti wa mitaa na vijiji kwa sababu ya matumizi mabaya ya mihuri kwa baadhi ya wenyeviti wa mtaa na vijiji nchini.

 Waziri (katikati), akijadiliana jambo na baadhi ya wenyeviti wa serikali za mitaa


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. George Boniphace Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wa Mkoa wa Dar es Salaam mara baada ya kumaliza mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu uamuzi wa Serikali wa kusitisha kwa muda katazo la Wenyeviti hao kutumia Mihuri ya Ofisi na badala yake utaratibu wa awali uendelee kutumika hadi hapo hatua nyingine zitakapochukuliwa. Wali muongozo huo uliotolewa na serikali uliwazuia wenyeviti hao kutumia mihuri hiyo na badala yake Afisa Mtendaji wa Kata ndiye mwenye mamlaka ya kjutumia mihuri hiyo, uamuzi ambao ulizua mtafaruku juzi kwenye mkutano baina ya wenyeviti hao na Mkuu wa wilaya ya Temeke.
(PICHANA: FRANK SHIJA – MAELEZO).
Reactions:

0 comments:

Post a Comment