Tuesday, 10 January 2017


NA JACQUILINE MRISHO.

IDARA ya Habari (MAELEZO) imebaini nyaraka za kughushi zilizowasilishwa na Mmiliki wa Kampuni ya FUKANI, Joseph Sheka wakati alipoziwasilisha kwa ajili ya kusajili gazeti la LETE MAMBO.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa MAELEZO, Dkt. Hassan Abbas, (pichani) amesema kuwa mtuhumiwa huyo aliwasilisha nyaraka mbalimbali akidai kuwa ni za Mamlaka ya Mapato (TRA) ambazo uchunguzi wa awali umebaini kuwa mihuri na sahihi za baadhi ya maafisa wa Mamlaka hiyo zilizotumiwa ni za kughushi.
“Ni vyema jamii ikafahamu kuwa huu sio wakati wa kujaribu kuishi kwa njia zisizo halali, kila mwananchi anapaswa kufuata taratibu zinatohitajika pindi anapotaka kupatiwa huduma katika maeneo mbalimbali ya ofisi za Umma.
Dkt. Abbas alitoa rai kwa ofisi mbalimbali za Umma kuwa makini na nyaraka zinazowasilishwa na wateja wao kwani zinaweza kuwa na malengo mbalimbali ya kuiingiza Serikali katika matatizo hivyo kuitia hasara.
Mbali na hayo Dkt. Abbas, alisisitiza kuwa wale wanaohisi waliwasilisha nyaraka zao na kuona kwamba zina utata kuja kuzirekebisha na watakaobainika kuwa walighushi nyaraka hizo sheria itafuata mkondo wake.
Kwa sasa Idara ya Habari imemkabidhi mtuhumiwa katika Kituo cha Polisi cha Kati jijini dar es salaam kwa mahojiano zaidi.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment