Wednesday, 11 January 2017


NA K-VIS BLOG/Khalfan Said
MBUNGE wa Kilombero, aliyehukumiwa kifungo cha miezi sita jela, Mh.Peter Lijualikali, (pichani juu), ataendelea na ubunge wake, mara amalizapo adhabu hiyo.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, (NEC), Bw. Ramadhan K.Kailima wakati akifafanua hatma ya ubunge wa mbunge huyo aliyehukumiwa kifungo hicho, Januari 11, 2017 baada ya mahakama ya wilaya ya Kilombero, kumkuta Mbunge huyo kijana, kuwa na hatia kufuatia mashtaka yaliyokuwa yakimkabili ya kufanya vurugu wakati wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo mwanzoni mwa mwaka 2016.
“Sheria inasema, Mbunge atakoma kuwa mbunge endapo atafungwa jela, zaidi ya miezi sita, sasa Mh. Lijualikali amehukumiwa kutumikia kifungo cha miezi sita jela, hivyo akimaliza kutumikia kifungo chake, ataendelea kuwa mbunge.” Alisema Bw. Kailima, wakati akihojiwa na Azam Two, kwenye taarifa yake ya habari.
Akifafanua zaidi, Bw. Kailima, alisema, kwa mujibu wa sheria hiyo, hata ingekuwa Mbunge huyo kafungwa kifungo cha nje cha zaidi ya miezi sita, bado angeendelea kuwa mbunge, kwani sheria hiyo inatamka kifungo cha zaidi ya miezi sita jela.
Kumekuwepo na hofu mitaani kuwa kufuatia adhabu hiyo ya kifungo, mbunge huyo tayari kapoteza ubunge wake.
Bw. Kailima alitolea mfano wa diwani mmoja kutoka huko Itilima, ambaye alihukumiwa kifungo cha miezi sita jela, na alipomaliza kutumikia adhabu hiyo ameendelea na udiwani wake, kwa hivyo, hata Mh. Lijualikali atakapomaliza adhabu hiyo, ataendelea kuwa mbunge, alifafanua Bw. Kailima.
Mbunge huyo anayo haki ya kukata rufaa mahakama za juu, ndani ya siku 30 tangu adhabu hiyo itolewe.

 Polisi wa kutuliza ghasia wakimburuta Mh. Peter Lijualikali, kutoka ukumbi wa ulikofanyika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kilombero, ambako yeye ni mjumbe
Mkurugenzi wa Uchaguzi, kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi, (NEC), Bw. Ramadhan Kailima
Reactions:

0 comments:

Post a Comment