Friday, 11 November 2016


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitoa heshima za mwisho kwa Spika Mstaafu, Samuel Sitta, bungeni mjini Dodoma, Novemba 11, 2016. (PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU)​

Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa  (wapili kulia) akimfariji mjane wa Spika Mstaafu Mama Margareth Sitta  baada ya mwili wa Spika Mstaafu, Marehemu Samuel Sita kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Dodoma Novemba 11, 2016.
Jeneza lenye mwili wa Spika Mstaafu, Samuel Sitta ukiingizwa bungeni mjini Dodoma Novemba 11, 2016
 NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID
WABUNGE wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Novemba 11, 2016, wamebubujikwa na machozi, wakati jeneza lenye mwili wa marehemu Samwel Sitta, “Mzee wa Kasi na Viwango” lilipowekwa kwenye jengo la bunge ili kutoa fursa ya wabunge kutoa maelezo ya kumbukumbu ya Mzee Sitta na kasha kutoa heshma za mwisho.
Miongoni mwa wabunge walioshindwa kujizuia wakati akiomba dua, ni Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt. Harrison Mwakyembe, ambaye pamoja na mambo mengine, kupitia maombi hayo alimwelezea spika Sitta kwamba alikuwa ni mtu mwenye msimamo na anayeipenda nchi yake na kuwapenda wanyonge lakini akichukizwa na “walafi” mafisadi.
Naye Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, na Mbunge wa Kigoma mjini, Zitto Kabwe, aliwataka wabunge na watanzania kwa ujumla kumuenzi Mee Sitta kwa vitendo, ambapo katika uongozi wake kama spika wa bunge la 9, alifanya mageuzi makubwa ya muundo wa bunge na utendaji kazi wake.
Akiongea kwa niaba ya CHADEMA, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, alimwelezea marehemu Sitta kama kiongozi aliyetoa fursa kwa demokrasia kuchanua.
Naye Kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe, aliwataka wabunge kudumisha upendo na heshima miongoni mwao bila ya kujali itikadi zao za vyama, na kubainisha kuwa wapinzani hawakumuelewa Mzee Sitta kama kweli ni mwana CCM kwa jinsi alivyowapa fursa ya kuzungumza bungeni na hata wakati mwingine kuwalazimisha mawaziri kujibu maswali kwa ufasaha.
Akizungumza kwa niaba ya wabunge wa CCM, Mh. Jason Rweikiza alimuelezea maehemu kuwa alikuwa ni mwa CCM mwaminifu aliyesaidia kukijenga chama na kukipatia heshima kubwa kutokana na uongozi wake imara.
Naye waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema serikali ilipokea kwa mshtuko mkubwa kifo cha marehemu Mzee Samwel Sitta, na mchango wake katika utumishi wa umma kamwe hautasahaulika.
Naye Spika wa bunge Job Ndugai, alimsifu marehemu kuwa hakuwa mtu mchoyo, aliwezesha kukuza vipaji vya wale waliokuwa chini yake na kutolea mfano yeye mwenyewe ambaye sasa ni spika kutoka nafasi ya uenyekiti wa bunge wakati wa uongozi wa marehemu Sitta, lakini pia Spika wa sasa wa bunge la Zanzibar na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera na watu wenye ulemavu), Mh. Jenista Mhagama ni miongoni mwa mafanikio ya Marehemu Sitta.
Akitoa wasifu wa marehemu, naibu Spika, Dkt. Tulia Ackson, alisema, marehemu Sitta alizaliwa tarehe 18/12/1942 huko Urambo mkoani Tabora, alipata elimu ya msingi mwaka 1950 katika shule ya msingi Urambo kabla ya kuahamia shule ya msingi Sikonge (Middle School), kutoka mwaka 1954 hadi 1957.
Marehemu Sitta, alijiunga na shule ya sekondari ya wavulana, Tabora Boys, mwaka 1958 alisoma kidato cha kwanza hadi cha sita na kuhitimu mwaka 1963.
1964 Marehemu alijunga na chuo kikuu cha Dar es Salaam ambako alisomea shahada ya sheria na kuhitimu mwaka 1971. Baada ya hapo alijiendelza kielimu kwenye vyuo mbalimbali vya ndani na nje.
Marehemu alifanya kazi mbalimbali serikalini na kwenye chama.
Marehemu ameacha mjane na watoto watano.
Marehemu Mzee Samwel Sitta, kama anavyojulikana kwa jina la Mzee wa “Kasi na Viwango” au Chuma cha Pua, anatarajiwa kuzikwa nyumbani alikozaliwa, huko Urambo, Jumamosi Novemba 12, 2016.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi AMIN.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika kikao maalum cha bunge cha kumuenzi Spika Mstaafu, Samuel Sitta, bungeni mjini Dodoma Novemba 11, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim  Majaliwa   akimfariji mjane wa Spika Mstaafu Mama Margareth Sitta  baada ya mwili wa Spika Mstaafu, Marehemu Samuel Sita kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Dodoma Novemba 11, 2016.
Waziri Mkuu Mstaafu, Samuel Malecela akimpa pole mjane wa Spika Mstaafu, Margareth Sitta bungeni mjini Dodoma Novemba 11, 2016
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka shada la maua kwenye jeneza la Spika Mstaafu Samwel Sitta, bungeni mjini Dodoma Novemba 11, 2016
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai pamoja na viongozi wengine wakiusubiri mwili wa Spika mstaafu, Samuel Sitta uteremshwe kwenye ndege katika uwanja wa ndege wa Dodoma Novemba 11, 2016

Mwili wa Spika Mstaafu Samuel Sitta ukiteremshwa kwenye uwanja wa ndege wa Dodoma Novemba 11, 2016
Reactions:

0 comments:

Post a Comment