Friday, 4 November 2016

Rais John Pombe Magufuli, akiongea na wahariri na waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaam, Novemba 4, 2016. (PICHA NA IKULU)

NA K-VIS MEDIA/KHALFAN SAID
RAIS John Pombe Magufuli, amesema kazi ya urais ni “adhabu” inahitaji kujitoa muhanga kwa vile ni kazi ngumu, na kuwataka Wahariri na Wananchi kumuunga mkono ili kuifikisha Tanzania mahala pazuri.
Rais aliyasema hayo wakati wa mkutao wake wa kwanza na wahariri na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam, Novemba 4, 2016, ikiwa ni mwaka mmoja tangu aapishwe kushika wadhifa huo Novemba 5, 2015.
“Kuwa katika kazi hii ni punishment, inahitaji sacrifice, ni kazi ngumu, nawashangaa wanaoililia, sikuja kufumua makaburi nataka nitengeneze nchi mpya, naomba wahariri na wananchi mnisaidie, walau baada ya miaka 5 tuwe tumefika mahala pazuri, mindset ya Watanzania lazima ibadilike”
Hata hivyo Rais alisema, hali ya uchumi kwa sasa ni nzuri lakini bado haijafikia mahala anapohitaji ifike na kuwataka Watanzania kuwa wavumilivu wakati serikali yake inajaribu kuweka mambo sawa.
Rais alizungumzia masuala mbalimbali ikiwemo uchumi, afya, elimu na miundombinu na kuonyesha matumaini yake kuwa utekelezaji wa ilani ya chama cha Mapinduzi ambacho yeye ndiye mwenyekiti wake itafanikiwa.
“Saa nyingine unalala saa 9 saa 10, unawaza mishahara nitalipaje, unaambiwa kuna mambo yanafanyika ovyo ovyo na wanaofanya ovyo ovyo unawajua, lakini inabidi kuyapokea na kusonga mbele.
Hawa wanaosema hela hazionekani mifukoni, na kama ni wafanyakazi mbona ninalipa mishahara kwa wakati, hebu muwaulize inakuaje hela zinakauka mifukoni wakati mishahara mnalipwa kama kawaida tena kwa wakati, yawezekana walikuwa wanapata pesa za ziada tena kwa njia haramu kwa vile mirija hiyo haramu imekwatwa ndio wanabaki wanalalamika.” Alisema.
Rais amesisitiza kuwa wakati wa “kupiga dili” umekwisha, na watu wasitarajie kuwa mbinyo huo utalegezwa au kubadilika, na kusisitiza msemo wake wa kuwataka watu kufanya kazi.
Rais alitolea mfano wa Watanzania wanaofaidi hali ya uchumi wa sasa ni wakulima wa Korosho mikoa ya kusini ambapo msimu uliopita waliuza Korosho zao kwa shilingi 1,000 kwa kilo lakini msimu huu wanalipwa shilingi 4,000 kwa kilo.
“Lazima tubadilike, inabidi tufanye kazi na niwaombe wanasiasa waweke maslahi ya taifa mbele, wasiwadanganye wananchi, siasa zitapita lakini Tanzania itabadi, ni lazima tuwasaidie wanyonge wa nchi hii, wavuvi, na wakulima ili waweze kuinua hali zao za maisha.” Alisema.
Akijibu swali kuhusu Katiba mpya, Rais Magufuli alisema, sio kwa sasa kuzungumzia swala hilo “Niache ninyooshe nchi, sikuwahi kutamka mahala popote wakati naomba kura, kuwa nitashughulikia masuala ya Katiba mpya,” alisema.
Akijibu swali kuhusu muswada wa Huduma za Habari za habari, Rais aliwaasa waandishi kuacha kuwasemea wenye vyombo vya habari kwa maslahi yao na kubainisha kuwa, kwa sasa swala hilo liko bungeni nay eye kamwe hazwezi kuingilia masuala ya muhimili mwingine. “Muswada huo tumeusubiri kwa miaka mingi sana tangu mimi nikiwa waziri, kwa kweli wanaosema haufai tunawajua tena wanatumia fedha kupinga swala hili, sasa mimi ninachoweza kusema, ukiletwa mezani kwangu baada ya kutoka bungeni, nitausaini siku hiyo hiyo.” Alisisitiza.
Aidha Rais amewalaumu wanasiasa kuwa wao ndio wanadhoofisha mabenki na mashirika kwa kuongoza kwa kukopa na kushindwa kurudisha fedha kwa wakati.
“Uchaguzi umekwisha, Rais ni John Pombe Magufuli, umpende usimpende, lakini Rais ni mimi, wapo pia wana CCM wa hovyo tu, tena wapiga dili, wapo, na mimi nitaendelea kupambana na mambo yote ya ovyo yaliyoko nchini.” Alisisitiza.
Mwandishi wa BBC, Sammy Awami, (kulia), aliuliza swali "Mh Rais, unatumia kigezo cha kuimarisha uchumi, kukandamiza demokrasia, hili unalizungumziaje.?, Rais Magufuli alikanusha kukandamzia demokrasia na kutolea mfano kuwa kama angekuwa anakandamiza demokrasia, upinzani wasingeshinda uchaguzi wa umeya Dar es Salaam na kwenye baadhi ya Manispaa za jiji.
Reactions:

0 comments:

Post a Comment