Friday, 4 November 2016

 Yang Fenglan,(66), akisindikizwa na askari magereza leo Novemba 4, 2016, kuelekea chumba cha mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam

NA K-VIS MEDIA/KHALFAN SAID
USIKILIZWAJI wa kesi ya kwanza ya uhujumu uchumi inayomkabili Raia wa China, Yang Fenglan,(66), umeshindikana kuanza leo Novemba 4, 2016 baada ya shahidi wa kwanza upande wa mashtaka,  kupatwa na dharura baada ya mke wake kuugua.
Badala yeke kesi hiyo itaanza kusikilizwa Novemba 15, 2016, baada ya Hakimu anayesikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi, Huruma Shaidi kukubaliana na upande wa mashtaka ulioongozwa na kiongozi wa mashtaka wa serikali, Faraja Nchimbi. “Mheshimiwa Hakimu, shahidi wetu wa kwanza ambaye ndiye angeeleza kwa kina kuhusu swala lililo mbele yetu, amepatwa na dharura, leo alifika ofisini kwetu na kutoa taarifa kuwa mkewe ni mgonjwa na asingeweza kushiriki vema katika kutoa ushahidi wake kwa vile ndiye anayewajibika kumsimamia, kwa hivyo ameomba aende kushughulikia suala hilo, na tunaiomba mahakama ipange kuanza kusikilizwa kwa kesi hii Novemba 15.” Alisema wakili huyo wa serikali Faraja Nchimbi.
Raia huyo wa China, anashtakiwa na watanzania wengine wawili, kwa tuhuma ya kuongoza na kufadhili mtandao mkubwa barani Afrika wa kusafirisha Meno ya Tembo, ambapo anadiwa kusafirisha meno 700 ya Tembo, yenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 2.5 kupeleka huko Mashariki ya Mbali.
Hata hivyo mama huyo wa Kichina ambaye aliwasili hapa nchini miaka ya 70 amekana mashtaka hayo na amerejeshwa rumande hadi tarehe iliyotajwa hapo juu. Vyombo vya habari vya China vimemuelezea mama huyo kuwa ndiye Mchina wa kwanza kujifunza lugha ya Kiswahili, ambapo alikuwa kama mkalimani wakati wa ujenzi wa reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), ujenzi uliofadhiliwa na Serikali ya China.

 Yang Fenglan,(66), akisindikizwa na askari magereza leo Novemba 4, 2016, kuelekea chumba cha mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam


Reactions:

0 comments:

Post a Comment