Sunday, 9 March 2014

Kikosi cha Yanga kilichojaribu kuvunja mwiko wa Waarabu kutofungwa na Yanga


Mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga, Jumapili usiku wa Machi 9, 2014, ilishindwa kulinda ushindi wake wa bao 1-0 dhidi ya National Al Ahly ya Misri, baada ya kukubali kichapo cha jumla ya mabao 4-3 yaliyofungwa kwa mikwaju ya penati.

Pambano hilo lililopigwa kwenye uwanja wa Max Alexandria, ulimalizika kwa Ahly kushinda bao 1-0 katika muda wa kawaida, ambao ulimaanisha kuwa sasa timu hizo zimetoshana nguvu na hapo ikaamuliwa mshindi apatikane kwa njia ya mikwaju ya Penati.

Mshambuliaji wa pembeni wa Ahly, Sayed Moawad ndiye aliyeleta msiba Yanga baada ya kufunga bao katika dakika ya 71 na hivyo kufufua matumainiya timu hiyo kubwa barani Afrika kuingia raundi ya 16 ya michuano ya soka barani Afrika kwa njia ya mikwaju ya penati.

Hata hivyo, vyombo vya habari vya Misri vimeiponda timu yao kwa kuonyesha mchezo usioridhisha na hivyo kuwatia homa mashabiki wake ambao hawakuruhusiwa kuingia uwanjani kutokana na sababu za kiusalama.

Vyombo hivyo vya habari vemeeleza kuwa katika kipindi cha kwanza, wachezaji wa Ahly walifika mara kadhaa kwenye lango la Yanga, lakini bila ya kuleta madhara makubwa.

Al Ahly sasa itakutana na  Ahly Bengazi ya Libya katika raundi ya 16, Ahly Bengazi walifanikiwa kuingia raundi hiyo baada ya kushinda  mabao 2-0 dhidi ya Berekum Chelsea ya Ghana mjini Bengazi.

Mshambuliaji hatari wa kimataifa wa Yanga, Emmanuel Okwi, alikuwa akilinda na mabeki wawili masaa yote na hivyo kumfanya asiweze kuonyesha makeke yake.

Baada ya kuona jahazi likienda mrama, kocha wa Ahly Mohamed Youssef, alimuingiza El-Sayed Hamdy, akichukua nafasi ya kiungo wa timu hiyo, Moussa Yedan.

Yanga katika kipindi cha pili ilicheza mchezo wa kujihami na hivyo kusababisha mashambulizi mfululizo na kunako dakika ya 71 Sayed Moawad, alipachika bao na hivyo kuwapa mtihani mgumu Yanga, ambao walihitaji sare tu ya bila kufungana au ya aina yoyote kusonga mbele kwenye michuano hiyo ya CAF.
Ilipowadia zamu ya mikwaju ya penati, Yanga ilifanikiwa kuingiza mikwaju mitatu ikifungwa na Nadir Haroub Canavaro, Didier Kavumbagu na Emmanuel Okwi, huku Oscar Joshua na mwenzake Said Bahanuzi, wakikosa penati zao.


Huendi kokote, hivi ndivyo vitendo vinavyojionyesha pichani, Emmanuel Okwi, akiwa amekumbatiwa asichomoke na mlizi wa Al Ahly, kwenye pambano la kwanza la michuano ya Ubingwa barani Afrika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, mapema mwezi huu. Yanga ilitolewa kwenye michuano hiyo baada ya kubanjuliwa mabao 4-3 kwa mikwaju ya penati.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment