Tuesday, 7 April 2020

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein na (kulia kwa Rais) Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe. Kassim Majaliwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wac Rais wa Zanzibar. Mhe. Mohammed Aboud Mohammed, Rais Mstaaf wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Amani Karume na (kushoto kwa Rais) Mkuu wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar Brigedia Jenerali Fahil Omar Nondo,wakiwa katika viwanja vya kaburi la marehemu Mzee Abeid Amani Karume. Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,wakati Kiongozi wa Dini Madhehebu ya Hindu Zanzibar.Pramuk Yoges akimuombea katika hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya kaburi la marehemu Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Jijini Zanzibar leo.7/4/2020.(Picha na Ikuklu)  
 RAIS  Mstaaf wa Zanzibar Zanzibar Mhe. Dkt. Amani Abeid Karume  akiwasili katika viwanja vya Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui kuhudhuria hafla ya Dua Maalum ya kumuombea Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, iliofanyika leo katika viwanja vya kaburi, akiwa ongozana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar. Mhe. Mohammed A
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein na (kulia kwa Rais) Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe. Kassim Majaliwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wac Rais wa Zanzibar. Mhe. Mohammed Aboud Mohammed, Rais Mstaaf wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Amani Karume na (kushoto kwa Rais) Mkuu wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar Brigedia Jenerali Fahil Omar Nondo,wakiwa katika viwanja vya kaburi la marehemu Mzee Abeid Amani Karume. Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,wakati Kiongozi wa Dini Madhehebu ya Hindu Zanzibar.Pramuk Yoges akimuombea katika hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya kaburi la marehemu Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Jijini Zanzibar leo.7/4/2020.(Picha na Ikuklu)  

 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa baada ya kumalizika kwa hafla ya Dua Maalum ya kumuombea Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, iliofanyika katika viwanja vya kaburi la marehemu katika viwanja vya Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu)


Monday, 6 April 2020


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Robert Masunya akiwa sambamba na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela wakipokea msaada kwa Meneja wa Benk ya NMB tawi la Iringa huku wakiwa na Tahadhari ya kujikinga na virusi vya Corona
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Robert Masunya akikabidhiwa msaada na kiongozi wa wauzaji wa vipuri vya magari mjini Iringa (Famari Stores)
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela akipeleka sehemu ya kuhifadhi msaada huo.

NA FREDY MGUNDA, IRINGA.
SERIKALI ya wilaya ya Iringa imepokea msaada wa chakula na sabuni kutoka kwa wauzaji wa vipuri vya magari mjini Iringa (Famari Stores) na Benki ya NMB kwa lengo la kuziwezesha baadhi ya kaya zilizokumbwa na mafuriko katika kitongoji cha Mbingama kijijini Isele, tarafa ya Pawaga wilayani Iringa kukabiliana na changamoto ya bidhaa hizo.
Msaada huo unaohusisha unga na maharage ulikabidhiwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela na wawakilishi wa taasisi hizo kwa nyakati tofauti mjini Iringa jana.
Akishukuru kwa msaada huo, Kasesela alisema; “unasafirishwa leo leo hadi kwa wahanga hao ili ukafanye kazi iliyokudiwa. Mahitaji ya vyakula na vitu vingine vya kibinadamu kwa wahanga wale ni makubwa na ya haraka.”
Kasesela alisema mafuriko yaliyotokea hivikaribuni katika kitongoji hicho yamesebabisha kaya 218 zenye jumla ya watu 801 kuachwa bila makazi huku akiba yao ya vyakula, fedha, nguo na vifaa vyao vingine vikisombwa baada ya nyumba zao kubomoka.
“Mahitaji ya kibinadamu kwawahanga hawa ni makubwa, tunaendelea kupokea misaada kutoka kwa wasamalia wema popote pale walipo na niishukuru kampuni ya Famari Stores na benki ya NMB kwa kusikia na kujitoa kuwasaidia wahanga hao,” alisema.
Wakati taarifa ya mwakilishi wa kampuni ya Famari Stores, Clement Kayage inaonesha msaada wao wa unga na sabuni una thamani ya zaidi ya Sh Milioni 1.5; meneja wa benki ya NMB tawi la Mkwawa, Komari Kiwia alisema msaada wao wa unga na maharage una thamani ya Sh Milioni 2.
Akikabidhi msaada huo, Kayage alisema; “Baada ya kupata taarifa za hali iliyowakuta wahanga hao, kampuni yetu iliguswa na kwa kuanzia tumetoa msaada wa unga na sabuni wenye thamani hiyo na tutakapopata nafasi tena basi tutaangalia chakusaidia.”
Naye meneja wa NMB alisema; “sisi kama taasisi tunayofanya kazi na jamii ya mkoa wa Iringa tumetoa unga na maharage, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh Milioni mbili kama mchango wetu unaolenga kuwafariji wahanga hao.”
Akiziomba taasisi zingine kujitokeza kuzisaidia kaya hizo Kasesela alisema serikali imeamua kuwaondoa moja kwa moja wahanga hao katika kitongoji hicho kwa kuwa rekodi zinaoneshwa kimekuwa kikikumbwa na mafuriko ya mara kwa mara.
“Kwahiyo kaya zote zimeondolewa katika kitongoji hicho cha Mbingama-hivyo hawataruhusiwa kurudi tena pale na serikali imekwishawapa maeneo mengine ndani ya  kijiji cha Isele kwa ajili ya kujenga makazi yao mapya,” alisema.
Alisema kuhamishwa kwa wananchi hao kumeongeza mahitaji yao vikiwemo vifaa vya ujenzi wa nyumba, vyakula, nguo na mahitaji mengine ya msingi ya binadamu.
“Msaada wa Famari Stores na NMB umekuja baada ya hivikaribuni kupokea msaada wa unga na nguzo za ujenzi kutoka kampuni ya Qwihaya General Enterprises ya mjini Mafinga,” alisema.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Robert Masunya aliwataja wengine waliotoa msaada kwa wahanga hao kuwa ni pamoja na world vision, msalaba mwekundu na taasisi mbalimbali za dini.
“Lakini na sisi kama halmashauri tumefanya juhudi kwa kupeleka unga, maharage, mafuta na maturubai kwa ajili ya kuwasitiri wahanga hao,” alisema.
Masunya alisema halmashauri yake pia imewapeleka wataalamu wa afya ili kuwasaidia wahanga hao kujikinga na magonjwa ya mlipuko ukiwemo ugonjwa wa corona unaooendelea kusambaa sehemu mbalimbali dunia.
NA MWANDISI WETU, SONGWE
Mkandarasi wa Mradi wa maji wa Iyula uliopo Wilaya ya Mbozi amezuiwa kutoka Nje ya Mkoa wa Songwe huku akiwekwa chini ya uangalizi wa jeshi la Polisi mpaka atakapo kamilisha vifaa na wataalamu watakaomalizia Mradi huo.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela ametoa zuio hilo leo mara baada ya kutembelea Mradi wa maji wa Iyula ambao ulitarajiwa kukamilika tangu mwaka 2017 huku ukiwa na thamani ya shilingi bilioni tano.
Brig. Jen. Mwangela amesema mkandarasi huyo anatakiwa aweke vifaa vyote na wataalamu wote watakao muwezesha kukamilisha ujenzi wa mradi huo ndipo ataruhusiwa kutoka nje ya Mkoa wa Songwe.
Ameongeza kuwa mkandarasi huyo aliweka masharti ya kupewa fedha nyingi ambapo tayari ameshapewa sehemu ya fedha hizo lakini bado utendaji wake wa kazi umekuwa wa kusuasua huku wananchi wakiendelea kupata adha ya kukosa maji.
Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Songwe Mhandisi Charles Pambe amesema mradi wa Maji wa Iyula una gharimu shilingi bilioni tano na tayari Mkandarasi ameshapewa bilioni 2.2
Mhandisi Pambe amesema kutokana na kusuasua kwa mkandarasi huyo RUWASA wana angalia uwezekano wa kuujenga mradi huo wenyewe kwa kutumia Force Account.
Naye Mkandarasi wa Mradi wa maji wa Iyula kutoka STC Construction ya Dar es Salaam Alan Makame amesema kusuasua kwa mradi huo ni kutokana na kucheleweshewa malipo pamoja na RUWASA kutotembelea mradi huo.
Amesema ndani ya siku tatu atakuwa ameanza kazi ya kuweka baadhi ya mabomba katika mradi huo na kuwa baada ya wiki mbili atakuwa amekamilisha mradi huo.
 Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wakikagua mabomba ya maji katika Mradi wa Iyula ambapo Mkuu wa Mkoa amemzuia Mkandarasi wa Mradi huo kutotoka Mkoa wa Songwe Mpaka atakapo kamilisha vifaa na wataalamu wote muhimu kwa ajili ya ukamilishaji wa Mradi huo.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela akizungumza wakati wa kukagua mabomba ya maji katika Mradi wa Iyula ambapo amemzuia Mkandarasi wa Mradi huo kutotoka Mkoa wa Songwe Mpaka atakapo kamilisha vifaa na wataalamu wote muhimu kwa ajili ya ukamilishaji wa Mradi huo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameitaka Kamati ya maafa ya Mkoa kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu kuanzia ngazi ya Kijiji, Mtaa, Kata, Tarafa hadi Mkoa huku akisisitiza mkazo wa kutolewa kwa elimu hiyo uelekezwe kwa vijana ambao wengi wao wanaonekana kutofuatilia taarifa za habari pamoja na elimu mbalimbali zinazotolewa na vyombo vya habari juu ya ugonjwa wa Corona.
Amesema kuwa vijana wa kisasa kuanzia mjini mapaka vijijini wamekuwa wagumu kusikiliza taarifa ya habari kwenye redio wala kuangalia taarifa ya habari kwenye runinga zaidi ya kujiendekeza kusikiliza muziki bila ya kujali na kutaka kujua serikali inasema nini juu ya kujikinga na maradhi hayo ya Corona.
“Akitembea kuna vitu viko masikioni humu anasikiliza muziki tu, nini serikali inasema kuhusu janga hili hajui, lakini mambo haya yanazungumwa sana kwenye redio, yanasemwa sana kwenye televisheni zetu, program ziko nyingi lakini vijana na kundi kubwa wanaonekana hawana muda wa kufuatilia, tuwarudishe hili kundi kubwa, lijenge tabia ya kufuatilia nini kinazungumzwa kwenye redio, kila redio inazungumza, ziko redio za ndani ziko redio zenye sura ya kitaifa,” Alisisitiza.
Aliongeza kuwa hii inaweza kuwa vita ya tatu ya dunia isipokuwa adui hatumuoni hivyo hatuna budi kila mmoja kwa nafasi yake akaendeleza kutoa elimu bila ya kuchoka ili kuweza kupambana na adui huyu ambaye haijulikani lini atashindwa.
Ameyaongea hayo wakati alipofanya kikao na kamati ya maafa ya mkoa iliyowajumuisha waganga wakuu wa wilaya wakiongozwa na mganga mkuu wa mkoa, viongozi wa dini na wataalamu wa ustawi wa jamii pamoja na maendeleo ya jamii wa mkoa na taasisi zisizo za kiserikali zinazojihusisha na kutoa elimu za afya katika mkoa.
Aidha, Alisisitiza ili kuweza kufanikisha kufikisha elimu kwa wananchi wote wa mkoa huo hakuna budi kuwaelimisha viongozi wa ngazi zote wakiwemo wenyeviti wote wa vijiji na mitaa ili watilie mkazo utekelezaji wa maelekezo ya serikali katika maeneo yao ya kiutawala.
Kuhusu ulinzi wa Mipakani Mh. Wangabo alisema kuwa Mkoa wa Rukwa una vipengo 50 katika ziwa Tanyanyika ambavyo hutumika na wananchi wan hi ya jirani ya Kongo na hivyo kuwataka wananchi kuwa makini na wavuvi wote wanaotoka katika nchi hiyo kuhakikisha wanawarudisha walikotoka na kisha kuripoti kwa vyombo vya usalama na kusisitiza kuwa wananchi wa maeneo hayo wanapaswa kuwa walinzi wa kwanza wa usalama wa nchi yetu.
 Maelezo ya Picha 
 Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akipimwa hali yake ya joto la mwili kabla ya kuingia katika ofisi za kituo cha Uhamiaji kilichopo katika mpaka wa Kasesya unaotenganisha nchi ya Tanzania na Zambia,uliopo kata ya Itete, Wilayani Kalambo.
 Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa maelekezo kwa maafisa wa uhamiaji pamoja na watumishi wa mpaka wa Kasesya unaotenganisha nchi ya Tanzania na Zambia kuhakikisha wananchi wanaotumia mpaka huo wanazingatia usafi.
 Afisa Afya wa Wilaya ya kalambo Richard Manuma (Kulia) akitoa maelezo juu ya maandalizia ya hema linalotumika kwaajili ya kuwaweka Karantini siku 14 wasafiri wanaotumia mpaka wa Kasesya unaotenganisha nchi ya Tanzania na Zambia katika Wilaya ya Kalambo mbele ya Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto).
Mkuu wa mkoa wa Rukwa na kamati yake ya Ulinzi na Usalama wakitoka katika geti (nyuma yao) linalotenganisha mpaka wa Tanzania na Zambia baada ya kutembelea mpaka huo na kujiridhisha juu ya udhibiti wa utumiaji wa mpaka huo kwa watanzania na wazambia. 
NA OWM, DODOMA
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa kote nchini kuimarisha ulinzi kwenye vituo vyote vilivyotengwa kwa ajili ya kuwaweka watu wote wanaoingia nchini(Karantini ya siku 14) na wahakikishe hakuna anayetoka ili kuepuka kusambaa kwa virusi vya corona.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo Aprili 6, 2020) wakati akizungumza na Wakuu wa Mikoa na Kamati zao za Ulinzi na Usalama za Mikoa ya Mipakani ya Arusha, Rukwa, Katavi, Dar Es Salaam, Tanga, Mtwara, Mara, Pwani, Ruvuma, Mwanza, Kilimanjaro, Mbeya, Kagera, Kigoma na Songwe kwa njia ya video conference.
Waziri Mkuu amesema kwa sasa takwimu zinaonyesha kuwa Aprili 5, 2020 kuliongezeka wagonjwa wawili Tanzania Bara na wawili Tanzania Zanzibar na hivyo kufanya idadi ya wagonja kufikia 24 Tanzania nzima ambapo jiji la Dar es Salaam lina idadi ya wagonjwa 12, wagonjwa 8 wapo Visiwani Zanzibar, Mkoani Kagera kuna mgonjwa 1 na mkoani Arusha kuna wagonjwa 2 na kwamba Serikali inaendelea kupokea sampuli za vipimo kutoka kwenye mikoa mbalimbali.
“Wagonjwa hawa wote ni wale waliotoka katika nchi mbalimbali, hivyo Wakuu wa Mikoa mnawajibu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na virusi vya corona hususani katika maeneo yanye mikusanyiko.” 
Waziri Mkuu amewataka viongozi hao waendelee kuimarisha ulinzi katika maeneo ya mipakani, viwanja vya ndege, bandarini na wahakikishe wageni wote wanaoingia nchini wanapelekwa kwenye maeneo maalumu yaliyotengwa kwajili ya kuangaliwa kama wanamaambukizi ya COVID-19. 
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa wasimamie na wahakikishe watoa huduma katika maeneo hayo wakiwemo walinzi wanapatiwa vifaa kwa ajili ya kujikinga ili wafanye kazi zao bila ya kuwa na mashaka.
“Imarisheni vituo na simamieni watu wasitoke kwenda mitaani na lazima washirikiane ili maambukizi yasizidi kusambaa nchini. Fuatilieni historia za watu wanaoingia nchini kuona maeneo waliyotembelea katika kipindi cha siku 14 kabla ya kuingia nchini.” 
Kwa upande wao Wakuu hao wa Mikoa wamesema wanaendelea kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Serikali kuhusu namna ya kukabiliana na virusi vya corona na kuhakikisha havisambai 
zaidi nchini.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza kwa njia ya video na Wakuu wa Mikoa  na Makatibu Tawala wa  Mikoa ya mipakani  kuhusu ugonjwa wa Corona akiwa ofisini kwake, Mlimwa jijini Dodoma, Aprili 6, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
NA OWM, DODOMA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hadi leo, hapa nchini kuna wagonjwa 24 waliothibitika kuwa na ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (COVID-19) ambapo watatu kati yao, wamepona na kuruhusiwa kutoka hospitali, mmoja amefariki dunia na wagonjwa 20 wanaendelea vema na matibabu.
“Serikali imeendelea kuwafuatilia watu 685 waliokutana na wagonjwa hao ambapo watu 289 wamemaliza siku 14 za kufuatiliwa na vipimo vyao vimethibitisha kuwa hawana maambukizi ya virusi vya Corona. Watu wengine 396 waliobaki wanaendelea kufuatiliwa ili kujiridhisha iwapo hawana maambukizi ya virusi hivyo.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Aprili 6, 2019) Bungeni jijini Dodoma kwenye mkutano wa 19 wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2020/2021.
Amesema hatua zinazochukuliwa katika kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona ni pamoja na kufanya ukaguzi (screening) kwa wageni wote wanaoingia nchini kutoka nje pamoja na kuwaweka katika uangalizi kwa siku 14.
“Ndege zetu tumezuia kufanya safari za nje, tumezuia wafanyakazi kwenda nje ya nchi, tumeimarisha mipaka sambamba na kuhakikisha wasafiri wote wanaoingia nchini wanalazimika kuwekwa chini ya uangalizi wa lazima kwa siku 14 kwa lengo la kudhibiti mienendo ya wasafiri chini ya ulinzi wa masaa 24,” amesema.
Waziri Mkuu amesema kutokana na umuhimu wa kuwatenga watu wanaofuatiliwa, Serikali imeagiza mikoa yote nchini itenge maeneo maalumu kwa ajili ya uangalizi na kujiridhisha iwapo hawana maambukizi.
“Hatua hii ni muhimu katika kudhibiti kuenea zaidi kwa maambukizi ya virusi vya Corona. Kayi ya hao, wengi ni wale waliotoka nje ya nchi. Maeneo hayo yametengwa kwa nia njema na yako kwa viwango tofauti kulingana na uwezo wa kifedha wa wahusika. Yako mabweni, ziko nyumba, na vyote vimewekwa kwa kuzingatia gharama mtu anayoweza kumudu,” amesisitiza.
“Tunafanya hivi ili kuondoa manung’uniko yaliyokuwepo kwamba watu wanapelekewa katika maeneo ambayo hawawezi kumudu. Na baada ya kuchukua hatua hizo, sasa hivi malalamiko hayo yamepungua.”
Akielezea hatua mbalimbali ambazo zinachukuliwa hivi sasa, Waziri Mkuu amesema Serikali inaimarisha maabara mbalimbali nchini ili ziweze kutoa huduma za upimaji ikiwemo maabara zilizopo kwenye mikoa ya Arusha, Dodoma Kigoma, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Pwani na Tanga.
“Hospitali za Rufaa za Kanda na Mikoa nazo zinaratibiwa kutoa huduma ya upimaji sambamba na maeneo ya mipakani. Shughuli hizo za upimaji zinafanyika kwa usimamizi wa Maabara Kuu ya Taifa ya Afya ya Jamii kwa lengo la kuthibitisha ubora wa vipimo hivyo na kuratibu utoaji wa matokeo.”
“Nilishasema atakayetoa taarifa za ugonjwa ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, na kama itabidi nitatoa mimi mwenyewe na kama italazimika sana atatoa Makamu wa Rais au Mheshimiwa Rais mwenyewe. Hii hali ya Wakuu wa mikoa na Wilaya kutoa matamko kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge hapa, haiku sawa.”
Waziri Mkuu amesema Tanzania imeendelea kushirikiana kwa karibu na Shirika la Afya Duniani (WHO), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) katika kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (COVID-19) na kwamba itaendelea kufanya tathmini kuhusu changamoto zinazoweza kusababishwa na ugonjwa huo na namna ya kuzitatua.
Bunge lilikubali kupitisha sh. 312,802,520,000 kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake kwa mwaka 2020/2021. Kati ya fedha hizo, sh. 88,429,156,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 224,373,364,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Vilevile, Bunge liliidhinisha sh. 121,786,257,000 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo kati ya hizo, sh. 113,567,647,000 ni za matumizi ya kawaida na sh. 8,218,610,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu hoja mbalimbali za wabunge wakati alipohitimisha hoja  kuhusu  Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2020/2021, Bungeni jijini Dodoma, Aprili 6, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu, George Mkuchika (kushoto) baada ya Bunge kupitisha Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2020/2021. Wa tatu kulia ni Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Augustine Mahiga, kulia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia , Profesa Joyce Ndalichako, na wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt  Angelina Mabula. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


 Boris Johnson.
NA K-VIS BLOG/Mashirika ya Habari
WAZIRI Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amepelekwa katika chumba cha kuhudumia wagonjwa mahututi baada ya afya yake kuzorota Jumatatu usiku Aprili 6, 2020, Ofisi yake imesema. Bw. Johnson alijiweka katika Karantini siku 10 zilizopita baada ya kupima na kukutwa na virusi vya Corona na Jumapili usiku alitoka kwenye karanini ya nyumbani na kupelekwa katika hospitali jijini Londona ambapo msemaji wa ofisi yake alisema ilikuwa ni hatua ya tahadhari baada ya ushauri wa daktari wake.
Kwa sasa Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Dominic Raab amechukua usukani kuongoza mapambano dhidoi ya ugonjwa wa COVID 19 wakati huu Bw. Johnson akiwa hospitalini. Waziri Boris ,mwenye umri wa miaka 55, amelazwa katika hospitali ya St Thomas mjini London.
"Ilipofika alasiri, hali ya Waziri Mkuu ilizorota na timu yake ya madaktari ikashauri ahamishiwe kwenye chumba cha wagonjwa mahtuti ili apate uangalizi wa karibu” Alisema msemaji wa ofisi ya Waziri Mkuu…..Waziri Mkuu anapata huduma bora kabisa na amewashukuru wafanyakazi wa Huduma za Afya (NHS) kwa kazi yao iliyotukuka.” Alisema msemaji huyo katika taarifa yake iliyotumwa kwa vyombo vya habari kwa njia ya email. (barua pepe).
Waziri Mkuu huyo wa Uingereza alipima na kukutwa na virusi vya COVID 19 vinavyosababosha  ugonjwa wa Corona Machi 26, 2020.